Hassan Nasrullah: Inasikitisha kuona bado kuna nchi zinaendeleza uhusiano na Israel
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i39209-hassan_nasrullah_inasikitisha_kuona_bado_kuna_nchi_zinaendeleza_uhusiano_na_israel
Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah nchini Lebanon sambamba na kuzitaka nchi zote za dunia kujiepusha kufanya uhusiano na utawala katili wa Israel, ameonyesha masikitiko kwamba bado kuna nchi zinaendeleza uhusiano na utawala huo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 20, 2018 01:12 UTC
  • Hassan Nasrullah: Inasikitisha kuona bado kuna nchi zinaendeleza uhusiano na Israel

Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah nchini Lebanon sambamba na kuzitaka nchi zote za dunia kujiepusha kufanya uhusiano na utawala katili wa Israel, ameonyesha masikitiko kwamba bado kuna nchi zinaendeleza uhusiano na utawala huo.

Sayyid Hassan aliyasema hayo jioni ya jana katika kumbukumbu ya kuwaenzi mashahidi wa eneo la Quneitra, kusini magharibi mwa Syria, iliyofanyika kusini mwa mji wa Bairut, Lebanon ambapo alisema kuwa kujiepusha kufanya mahusiano na utawala wa Kizayuni ni kati ya mapendekezo muhimu yaliyotolewa pia na nchi za Kiarabu, ambayo hata hivyo baadhi ya nchi za Kiarabu zimeshindwa kuyatekeleza. Sayyid Nasrullah amefafanua kuwa, Lebanon imefungamana vilivyo na pendekezo hilo, kwa kuacha kufanya mahusiano na utawala huo khabithi na kwamba Walebanon hawana msamaha wowote katika uwanja huo.

Saudia na Israel bado zinaendeleza mahusiano 

Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah nchini Lebanon sambamba na kuwaenzi mashahidi wa eneo la Quneitra, amesema kuwa, lau kama si kujitolea wanamuqawama wa Hizbullah, usalama na amani inayoshuhudiwa leo nchini Lebanon, isingekuwepo. Kadhalika ameashiria tuhuma za hivi karibuni za serikali ya Marekani dhidi ya harakati hiyo kwamba eti inajihusisha na biashara ya madawa ya kulevya na kuongeza kuwa, tuhuma hizo hazina msingi wowote na zinafanyika kupitia njama chafu za Washington dhidi ya harakati hiyo ya Kiislamu. Amebainisha kwamba, kwa mujibu wa msingi wa harakati hiyo, madawa ya kulevya ni haramu. Katika hatua nyingine Sayyid Nasrullah sambamba na kukosoa msimamo wa hivi karibuni wa viongozi wa Marekani juu ya kubakisha askari wa Marekani nchini Iraq na Syria kwa kisingizio cha 'kuzuia kurejea kundi la Daesh' ameutaja msimamo huo kuwa ni unafiki na undumakuwili wa wazi wa Marekani.

Askari vamizi wa Marekani nchini Iraq

Akiashiria upinzani mkali wa serikali ya Iraq juu ya kuwekwa kambi za kijeshi za Marekani nchini humo kwa kisingizio cha kupambana na genge la Daesh ameongeza kuwa, ni Marekani yenyewe ndiyo iliyounda kundi hilo kwa lengo la kuhalalisha kurejea katika eneo la Mashariki ya Kati hususan Iraq. Amefafanua kwamba jeshi la Iraq na Syria halitoruhusu suala hilo tena.