Czech kuuhamishia ubalozi wake Quds chini ya mashinikizo ya Israel
Jamhuri ya Czech ipo chini ya mashinikizo ya utawala wa Kizayuni wa Israel ya kuitaka ihamishie ubalozi wake katika mji wa Quds Tukufu (Jerusalem) kama ilivyofanya Marekani.
Kanali ya 10 ya televisheni ya Kizayuni imemnukuu Daniel Meron, balozi wa utawala haramu wa Israel mjini Prague akisema mashinikizo hayo ya kuitaka Jamhuri ya Czech iuhamishie ubalozi wake Baitul Muqaddas yametokana na hatua ya Guatemala kutangaza kuwa itauhamishia ubalozi wake Quds kutoka Tel Aviv.
Hata hivyo balozi huyo wa Kizayuni amesisitiza kuwa, uamuzi wa mwisho kuhusu kadhia hiyo utatolewa na Andrej Babis, Waziri Mkuu wa Czech, ambaye huenda akawa kikwazo.
Mwishoni mwa mwaka jana, Rais Jimmy Morales wa Guatemala alitangaza kuwa nchi hiyo ndogo ya Amerika ya Kati itauhamishia Quds ubalozi wa nchi hiyo ulioko Tel Aviv, ikiwa ni nchi ya kwanza kufuata kibubusa nyayo za Rais Donald Trump wa Marekani.
Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Palestina ilisema hatua hiyo ya serikali ya Guatemala ya kupuuza azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa juu ya mji huo mtukufu ni jambo la kufedhehesha na kinyume cha sheria za kimataifa.
Disemba 6 mwaka jana, Trump alitangaza kuwa eti Quds ni mji mkuu wa utawala haramu wa Israel, hatua ambayo imepingwa na kulaaniwa vikali na aghlabu ya nchi duniani na taasisi za kimataifa likiwemo Baraza la Usalama na Baraza la Kuu la Umoja wa Mataifa.