Mtazamo wa Hassan Nasrullah kuhusiana na uchaguzi wa bunge nchini Lebanon
Jumapili iliyopita Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya nchini Lebanon alihutubia eneo la Nabatieh kusini mwa Lebanon ambapo alibainisha maoni yake kuhusiana na uchaguzi ujao wa bunge nchini humo.
Uchaguzi umepangwa kufanyika tarehe sita Mei mwaka huu. Uchaguzi wa mwisho wa bunge nchini Lebanon ulifanyika mwaka 2009 ambapo kwa kipindi cha miaka tisa sasa nchi hiyo haijashuhudia tena uchaguzi mwingine. Ni kwa ajili hiyo ndio maana bunge la sasa likaongezewa mihula mitatu ya kuwa madarakani wa kwanza ukiwa ni wa mwezi Juni 2013 ambapo liliongezewa miezi 17, mwezi Novemba 2014 miezi 31 na mwezi Juni 2017 miezi 17.
Ni mazingira hayo ndiyo yamepelekea uchaguzi wa bunge wa mwaka huu kuwa na umuhimu wa aina yake. Aidha harakati ya Hizbullah ya Lebanon ni yenye nafasi muhimu katika muundo wa utawala wa nchi hiyo ambapo chama cha Muungano wa Machi 8 chenye mfungamano na harakati hiyo ya Kiislamu na kadhalika chama cha Muungano wa Machi 14, ni mirengo miwili shindani katika uchaguzi huo ujao. Harakati ya Hizbullah inashiriki uchaguzi huo kwa orodha ya mrengo uliopewa jina la 'Matumaini na Uaminifu'. Katika orodha hiyo, wagombea 13 wenye mafungamano na harakati hiyo wameungana na wagombe wa chama cha Amal pamoja na vyama na shakhsia walio karibu na mirengo hiyo miwili ambapo watatoa orodha ya pamoja ya vituo tofauti vya muungano wao. Kongamano la siku ya Jumapili eneo la Nabatieh ambalo Sayyid Hassan alilihutubia, lilikuwa na lengo la kuunga mkono orodha hiyo ya "Matumaini na Uaminifu".
Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah alibainisha umuhimu wa kushiriki katika uchaguzi huo na kusema kuwa, bunge ni mama wa asasi na mihimili yote nchini Lebanon na kwamba, kulifanyia mabadiliko ni suala muhimu, kwani ni muhimili pekee ambao unaweza kuifanyia mabadiliko katiba bila hata ya kuitisha kura ya maoni. Kwa ajili hiyo, sisitizo la umuhimu wa kushiriki katika uchaguzi huo, ni nukta ya kwanza iliyoashiriwa katika hotuba ya Sayyid Hassan Nasrullah. Nukta muhimu ni hii kwamba, uchaguzi ujao wa Lebanon una taathira katika matukio ya eneo la Mashariki ya Kati, suala ambalo pamoja na mambo mengine linabainisha nafasi kubwa ya taifa hilo katika matukio ya eneo. Umuhimu huo pia unatokana na nafasi chanya ya Hizbullah katika muundo wa ndani ya Lebanon na muundo wa nguvu katika eneo la Mashariki ya Kati.
Hakuna shaka kwamba, Hizbullah imesaidia katika kuwashinda magaidi nchini Syria na kadhalika kusambaratisha mipango na njama za madola ya kigeni kwa ajili ya kuiondoa madarakani serikali halali ya Damascus chini ya Rais Bashar al-Assad wa nchi hiyo. Ukweli ni kwamba mafanikio ya harakati ya Hizbullah katika kuwashinda magaidi, ni katika mkondo uleule wa mafanikio ya muongo uliopita katika kukabiliana na utawala haramu wa Israel. Mafanikio hayo makubwa ya Hizbullah ndiyo yamesababisha kuongezeka hujuma na njama mbalimbali za maadui dhidi ya harakati hiyo. Katika uwanja huo, Jumapili iliyopita Sayyid Hassan Nasrullah alisema: "Moja ya malengo muhimu ya matukio ya Syria ni kutoa pigo kwa muqawama na maudhui hatari zaidi katika pigo hilo dhidi ya muqawama ni kuanzisha vita vikubwa vya ndani kati ya jeshi la serikali na wanamuqawama wa Hizbullah." Mwisho wa kunukuu. Suala la kuiweka kando na ulingo wa kisiasa harakati ya Hizbullah nchini Lebanon na katika muundo wa nguvu wa eneo la Mashariki ya Kati limefikia hatua ambayo wapinzani wake mbali na kuchochea vita vya ndani ya Lebanon, wanapanga hata njama za kutaka kuishambulia kijeshi nchi hiyo ya Kiarabu.
Kuhusiana na suala hilo, Nasrullah anasema tena: "Hatari kubwa zaidi iliyoratibiwa kwa ajili ya kutoa pigo kwa muqawama, ni kuibua vita vya ndani ili jeshi la serikali liweze kukabiliana na muqawama. Hata hivyo wamebaini kwamba jeshi la Lebanon halitoingia katika vita hivyo dhidi ya muqawama. Na ni kutokana na hilo ndipo haraka wakaanzisha vita vya mwaka 2006." Mwisho wa kunukuu. Hakuna shaka kwamba, sababu ya kuongezeka hujuma za kila upande za wapinzani wa Hizbullah hususan utawala haramu wa Kizayuni, Marekani na Saudia dhidi ya harakati hiyo ya Kiislamu nchini Lebanon ni kudhihiri haraka harakati nyingine za Kiislamu kama hiyo katika eneo, ikiwemo Harakati ya Wananchi wa Iraq ya Hashdu sh-Sha'bi na Answarullah ya nchini Yemen.