Nasrullah: Israel imejichimbia kaburi kwa kuishambulia kijeshi Syria
Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya nchini Lebanon amesema utawala wa Kizayuni wa Israel umefanya makosa makubwa zaidi kwa kuwashambulia wanajeshi wa Iran ulipolenga kituo cha anga cha Syria hivi karibuni.
Akihutubu kupitia njia ya televisheni mjini Beirut jana Ijumaa, Sayyid Hassan Nasrullah amesema kuwa, "Utawala wa Kizayuni umefeli katika mahesabu yake na umefanya kosa la kihistoria kwa kuwashambulia wanajeshi wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Syria. Lazima watambue kuwa Iran sio taifa dhaifu na lenye woga."
Amebainisha kuwa, utawala huo wa Kizayuni unatoa kauli za kukinzana kuhusu hujuma hiyo na hata kudai kuwa halikuhusika, kwa kuwa unaogopa matokeo yake mabaya.
Utawala wa Kizayuni Jumatatu iliyopita ulikishambulia kituo cha anga cha T-4 huko Syria na kuua watu kadhaa wakiwemo wanajeshi wa Iran. Utawala huo haramu kama vile Marekani na baadhi ya nchi waitifaki wake zikiwemo Uingereza na Ufaransa, umeituhumu serikali ya Damascus kuwa imehusika na shambulio la kemikali katika mji wa Douma kwa kutegemea taarifa za uwongo kutoka kwa magaidi wa Jayshul Islam bila hata ya kuwa na ushahidi na nyaraka zenye kuthibitisha jambo hilo.
Kwengineko katika hotuba yake, Sayyid Nasrullah amesema vitisho vya Rais Donald Trump wa Marekani kamwe havitaibabisha Syria, wala Iran wala Russia. Amesema vitisho hivyo vinalenga kuutia wasi wasi moyo wa kimuqawama wa wananchi wa eneo hili.
Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya nchini Lebanon amesema Trump ni mfanyabiashara ambaye ameligeuza jeshi la Marekani kuwa kikosi cha mamluki. Ameongeza kuwa, dunia ipo hatarini kwa uwepo wa mtu kama Trump ambaye kaulimbiu yake inasema, "Ukinilipa, nitatekeleza shambulizi lolote au kuanzisha vita kwa niaba yako."