Wanawake wahajiri wa Kiafrika wanadhalilishwa kingono katika jela zinazosimamiwa na Saudia na UAE, Aden
(last modified Thu, 19 Apr 2018 07:51:48 GMT )
Apr 19, 2018 07:51 UTC
  • Wanawake wahajiri wa Kiafrika wanadhalilishwa kingono katika jela zinazosimamiwa na Saudia na UAE, Aden

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR yameripoti kuwa wanawake wahajiri wa Kiafrika wanakashifiwa na kudhalilishwa kingono katika mji wa Aden kusini mwa Yemen ambao unadhibitiwa na vikosi vya Imarati (UAE) na Saudi Arabia.

Baada ya kuwahoji wahajiri kutoka Ethiopia, Somalia na Eritrea katika eneo la Al-Bariqah lililoko kwenye mji wa Aden unaodhibitiwa na vikosi vinavyoungwa mkono na Imarati vyenye mfungamano na Abd Rabbuh Mansour Hadi, rais wa Yemen aliyejiuzulu, shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limebaini kuwa wahajiri hao wameteswa na kudhalilishwa kimwili walipokuwepo mahabusu.

Human Rights Watch limeashiria kuendelea ufuska mkubwa unaofanywa na walinzi wa jela wanaoungwa mkono na Imarati dhidi ya wanawake, wasichana na hata watoto wadogo na kueleza kwamba: mahabusu wawili waliamua kujiua kwa kujipiga risasi kutokana na kuendelea vitendo vya ukatili vinavyofanywa na maafisa wa jela.

Wahajiri wa Kiafrika kutoka Somalia walioko nchini Yemen

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi limeashiria maelezo ya wahajiri wa Kiafrika walionusurika na ukatili, ubakaji, kunyongwa na kufa kwa njaa na kubainisha kuwa: maafisa wenye mfungamano na Mansour Hadi katika mji wa Aden wamewanyima watu wanaoomba hifadhi haki yao ya kusaidiwa kama wakimbizi na kuwafanya walazimike kurudi wanakotoka kwa kutumia njia hatarishi ya baharini.

Maafisa wa Aden wanayazuia mashirika ya kimataifa kuingia katika mji huo ili kuandaa ripoti kuhusu hali mbaya na ya kusikitisha waliyonayo wahajiri.

Matukio yanayojiri kusini mwa Yemen yanaonyesha hitilafu na tofauti ambazo zimeshadidi kati ya Saudi Arabia na Imarati juu ya kujijengea satua na ushawishi ndani ya Yemen huku kila mmoja akijaribu kumuondoa mwenzake nchini humo.../

Tags