Hizbullah: Mashambulizi ya Israel Syria yatawasha moto katika eneo zima
Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Harakati ya Kiislamu ya Hizbullah ya nchini Lebanon sambamba na kuielezea kuwa nyeti hali ya hivi sasa katika eneo la Mashariki ya Kati amesema kuwa, kuendelea mashambulizi ya Israel dhidi ya Syria si tu kwamba kunahatarisha usalama wa nchi hiyo, bali kuna hatari yatazusha mgogoro katika eneo zima.
Sayyid Hassan Nasrullah ameyasema hayo jioni ya jana kupitia hotuba aliyoitoa kusini mwa Bairut, mji mkuu wa Lebanon ambapo sambamba na kufafanua matukio ya eneo hili amesema kuwa, hali ya hivi sasa imefikia kiasi kwamba maadui wakiongozwa na Marekani na utawala haramu wa Israel na kwa madai tofauti, wanakusudia kuifanya Mashariki ya Kati kuwa na hali mbaya zaidi na kuwasha moto wa vita kati ya nchi za eneo hili lote.
Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ameashiria mashambulizi ya mara kwa mara ya anga na mizinga yanayofanywa na utawala katili wa Kizayuni dhidi ya Syria hususan katika wiki za hivi karibuni na kusema kuwa, Wazayuni kwa uungaji mkono wa Marekani wanakusudia kupanua mzozo zaidi nchini Syria na katika nchi nyingine za eneo hili na amezitaka nchi hizo kuwa macho. Akizungumzia kushindwa mtawalia kwa makundi ya kigaidi kama vile Daesh (ISIS) nchini Syria na Iraq kulikopelekea kuchanganyikiwa waungaji mkono wao hususan Marekani, Israel na Saudia, amesema kuwa, ni kwa ajili hiyo ndio maana maadui wameanzisha uchochezi kwa kuupanua mgogoro wa Syria na kuuingiza kwenye mataifa mengine ya eneo hili.
Kadhalika Sayyid Hassan Nasrullah, amezungumzia matukio ya uchaguzi wa bunge nchini Lebanon na kusema, lau kama si juhudi za wanamuqawama wa Hizbullah na jeshi la nchi hiyo za kupambana na genge la Daesh katika mipaka yake, hii leo Lebanon isingeshuhudia maandalizi ya uchaguzi huo. Uchaguzi wa bunge nchini Lebanon umepangwa kufanyika tarehe sita ya mwezi ujao. Aidha ameongeza kuwa: "Tunataka mshikamano na ushiriki wa kweli wa Waislamu na Wakristo katika uchaguzi huo kwa kuwa fikra za ubaguzi nchini Lebanon zimekwisha na kwamba chama ambacho kinataka kipate kila kitu, kamwe hakitofanikiwa." Amesema Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu wa Harakati ya Kiislamu ya Hizbullah ya nchini humo.