Sayyid Hassan Nasrullah: Ni ujinga wa hali ya juu kuiamini Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i44484-sayyid_hassan_nasrullah_ni_ujinga_wa_hali_ya_juu_kuiamini_marekani
Katibu Mkuu wa Harakati ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon ameashiria kitendo cha Marekani cha kuvunja mikataba na maazimio ya kimataifa na kusema kuwa, baada ya tajriba zote ambazo zimeshuhudiwa kwa Washington, ni ujinga wa hali ya juu kuiamini nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 14, 2018 12:55 UTC
  • Sayyid Hassan Nasrullah: Ni ujinga wa hali ya juu kuiamini Marekani

Katibu Mkuu wa Harakati ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon ameashiria kitendo cha Marekani cha kuvunja mikataba na maazimio ya kimataifa na kusema kuwa, baada ya tajriba zote ambazo zimeshuhudiwa kwa Washington, ni ujinga wa hali ya juu kuiamini nchi hiyo.

Sayyid Hassan ameyasema hayo jioni ya leo katika marasimu ya kumbukumbu ya mwaka wa pili wa kuuawa shahidi Mustafa Amin Badruddin, maarufu kwa jina la 'Sayyid Dhulfiqaar' huko kusini mwa mji wa Bairut, mji mkuu wa Lebanon ambapo pamoja na mambo mengine amebainisha kwamba, matukufu yoyote ya kibinaadamuu hayana umuhimu hata kidogo mbele ya maamuzi ya Marekani.

Bendera za utawala haramu wa Israel na Marekani

Amesisitiza kuwa, kitu cha kwanza kinachozingatiwa kwa daraja ya kwanza na Washington ni maslahi yake binafsi na kisha maslahi ya utawala khabithi wa Kizayuni. Katibu Mkuu wa Harakati ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon ameashiria operesheni za hivi karibuni zilizofanywa na jeshi la Syria katika miinuko ya Golan inayokaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Israel na kuongeza kuwa, kile kilichojiri katika tukio hilo ni moja ya majibu madogo kwa uvamizi na chokochoko za Israel dhidi ya Syria na kwamba ujumbe wa operesheni hizo za jeshi la Syria kwa utawala huo ni kwamba, Israel haiwezi kutoka eneo la Mashariki ya Kati bila kupata jibu. Amesema kuwa, utawala huo umefahamu kwamba jibu la pili litakalotolewa na upande wa muqawama juu ya chokochoko zake, halitakuwa katika milima ya Golan, bali litaenda ndani ya Israel moja kwa moja na kwamba ni Tel Aviv ndio iliomba  radhi na kutaka kusimamishwa mashambulizi yaliyopita. Aidha ameashiria mpango unaoitwa 'Muamala wa Karne' ambao unatajwa na baadhi ya nchi za Kiarabu kuwa eti ndio njia ya utatuzi ya Marekani kwa kadhia ya Palestina na kusema kuwa, mpango huo ni changamoto kubwa ambayo walimwengu wote wanatakiwa kuitupilia mbali.

Saudia ambayo imejiegemeza kwa kila kitu kwa Marekani

Ameenda mbali zaidi na kusema kuwa nchi yoyote inayoegemeza mustakbali wake kwa Marekani sambamba na maamuzi yake kuitegemea Washington, basi inafanya kosa kubwa. Amelitaka taifa la Lebanon na Wapalestina kupata ibra kutokana na mienendo hasi ya serikali ya Marekani ikiwemo hatua ya kufungua ubalozi wake mjini Quds na kufafanua kuwa, kamwe Marekani haifungamani na mikataba wala maazimio ya kimataifa katika hali ambayo ni nchi hiyo hiyo inazitaka nchi nyingine kuheshimu mikataba hiyo.