Vikwazo vya Marekani dhidi ya viongozi wa Hizbullah ya Lebanon
Serikali ya Marekani imetangaza vikwazo vingine vipya, mara hii ikiwa ni dhidi ya viongozi waandamizi wa Hizbullah ya Lebanon akiwemo Katibu Mkuu wake Sayyid Hassan Nasrullah na naibu wake Sheikh Naeem Qassim.
Kwa mujibu wa tangazo lililotolewa siku ya Jumatano ya tarehe 16 Mei na Idara ya Wizara ya Fedha ya Marekani inayohusika na udhibiti na ufuatiliaji wa milki za kigeni, shakhsia sita wamejumuishwa kwenye orodha ya vikwazo kwa tuhuma ya kile kilichotajwa kama eti kuwa na uhusiano na ugaidi wa kimataifa; watano kati ya shakhsia hao sita ni viongozi waandamizi wa Hizbullah ya Lebanon.
Ijapokuwa kabla ya hapo serikali ya Marekani ilikuwa imeyaweka majina ya baadhi ya viongozi wa Hizbullah akiwemo Sayyid Hassan Nasrullah kwenye orodha ya vikwazo, lakini hatua iliyochukuliwa siku ya Jumatano ni kiashiria cha awamu mpya ya mkakati wa serikali ya Trump kuhusu Hizbullah na mhimili wa muqawama, mkakati ambao una umuhimu mkubwa kwa kuzingatia wakati wa kutekelezwa kwake.
Nukta ya kwanza kuhusiana na mkakati huo ni kwamba vikwazo vipya dhidi ya viongozi na wanachama waandamizi wa Hizbullah vimewekwa baada ya kupita siku kumi tu tangu ulipofanyika uchaguzi wa bunge nchini Lebanon. Katika uchaguzi huo, muungano wa Hizbullah ulinyakua viti 67 na kuwa mrengo wenye viti vingi zaidi katika bunge lijalo la Lebanon. Ushindi huo mkubwa ulibeba ujumbe muhimu, ambao ni kuzidi kuwa na sauti na ushawishi mrengo wa muungano wa Hizbullah katika muundo wa nguvu na madaraka nchini humo. Hatua ya serikali ya Marekani ya kuwawekea vikwazo viongozi waandamizi wa Hizbullah ni jibu na radiamali kwa matokeo ya uchaguzi huo wa bunge kwa kuonyesha jinsi Washington ilivyochukizwa na matokeo hayo na wakati huohuo kufanya uafriti wa kukwamisha uendeshaji wa masuala ya ndani ya Lebanon.
Nukta nyingine ni kwamba hatua hiyo ya serikali ya Marekani imechukuliwa siku mbili tu tangu ubalozi wa nchi hiyo uondolewe Tel Aviv na kuhamishiwa Baitul Muqaddas. Zoezi la kuhamishwa ubalozi huo limefanyika katika hali ambayo askari wa Israel wamewaua shahidi Wapalestina zaidi ya 65 na kuwajeruhi wengine wapatao 3,800 katika operesheni ya kukandamiza maandamano makubwa yaliyofanywa Siku ya Nakba sambamba na kuhamishwa ubalozi wa Washington. Hatua hiyo imechukuliwa ili kusisitiza kwamba Marekani inaunga mkono hatua zinazochukuliwa na Israel ikiwemo ya jinai ya mauaji ya kinyama iliyofanya hivi karibuni.
Isisahaulike pia kwamba serikali ya Washington imechukua hatua hiyo wiki moja tu baada ya nchi hiyo kujitoa kwenye makubaliano ya nyuklia na Iran. Moja ya malengo muhimu zaidi ya Marekani kujitoa kwenye makubaliano ya JCPOA ni kuzuia kuwa na nguvu zaidi vuguvugu la muqawama katika eneo la Magharibi ya Asia. Kumwekea vikwazo kiongozi na wanachama waandamizi wa Hizbullah ya Lebanon, nako pia kumefanyika katika muelekeo huo na kwa lengo la kuishinikiza Hizbullah ambayo ni muitifaki muhimu zaidi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katka eneo.
Baada ya Trump kutangaza kuwa Marekani imejitoa kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, utawala haramu wa Israel uliishambulia Syria kwa makombora, hujuma ambayo ilikabiliwa na jibu la jeshi la nchi hiyo; na kama alivyoashiria Sayyid Hassan Nasrullah katika hotuba aliyotoa siku ya Jumatatu iliyopita, makombora 55 yalifyatuliwa kuelekea miinuko ya Golan inayokaliwa kwa mabavu. Katika hotuba yake hiyo, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon mbali na kuuonya utawala wa Kizayuni na kusisitiza kwamba mvuto wa makeke yake na wa jeshi lake la anga umekwisha alisema: "Ikiwa uchokozi wa Israel dhidi ya Syria utaendelea, jibu la mara hii litalenga kwenye kitovu cha Palestina inayokaliwa kwa mabavu na wala si Golan." Uamuzi uliotangazwa siku ya Jumatano na serikali ya Marekani wa kumwekea vikwazo kiongozi na wanachama waandamizi wa Hizbullah ya Lebanon, umechukuliwa zikiwa zimepita siku mbili tu tangu Sayyid Hassan Nasrullah atoe onyo hilo kali kwa utawala haramu wa Kizayuni; na inavyoonekana ni hatua ya kukabiliana na msimamo huo madhubuti na onyo hilo lisilo na chembe ya mzaha alilotoa Katibu Mkuu huyo wa Hizbullah.../