Palestina yaitaka UN ichunguze mauaji yanayofanywa na Israel huko Gaza
Balozi wa Palestina katika Umoja wa Mataifa ametoa mwito kwa Baraza Kuu la umoja huo kukumbatia azimio linalotaka kuchunguzwa jinai za kutisha zinazoendelea kufanywa na wanajeshi katili wa Israel dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.
Riyadh Mansour aliyasema hayo jana Ijumaa katika kikao na waandishi wa habari mjini New York, saa chache baada ya wanajeshi hao wa Kizayuni kuua shahidi Wapalestina wengine wanne, waliokuwa wakishiriki maandamano ya amani ya Siku ya Quds katika mpaka wa Gaza.
Shirika la habari la AFP limenukuu duru za kidiplomasia zikisema kuwa, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limeitisha kikao cha dharura Jumatano ijayo kujadili kadhia ya Gaza, kufuatia mashinikizo kutoka Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu.
Kadhalika balozi huyo wa Palestina katika UN amesisitiza kuwa, lazima watenda jinai wote wa Israel wakabiliwe na mkono wa sheria kutokana na ukatili walioufanya na wanaoendelea kufanya dhidi ya Wapalestina.
Duru za habari zinadokeza kuwa karibu Wapalestina 280,000 walishiriki katika Sala ya Ijumaa katika Msikiti wa al-Aqsa hiyo jana.
Tangu tarehe 30 Machi mwaka huu hadi hivi sasa, wanajeshi katili wa Israel wameshaua shahidi Wapalestina wasiopungua 130 katika maandamano ya amani yaliyoanza wakati wa maadhimisho ya mwaka wa 42 wa "Siku ya Ardhi" ambapo pia maelfu ya Wapalestina wamejeruhiwa.