Kushikilia Bahrain rekodi ya wafungwa wa kisiasa ulimwenguni
Jalal Firouz, mbunge wa zamani wa Bahrain na mmoja wa wanaharakati wa masuala ya haki za binadamu wa nchi hiyo amesema, kwa sasa Bahrain ndio inayoshika nafasi ya kwanza ulimwenguni kwa kuwa na wafungwa wengi wa kisiasa.
Takwimu zinaonyesha kuwa, Bahrain ina zaidi ya wafungwa wa kisiasa elfu tano. Kwa kuzingatia idadi ndogo ya watu iliyonao, nchi ya Bahrain ina wafungwa wengi wa kisiasa kuliko nchi yoyote ile ulimwenguni. Utawala wa Aal-Khalifa umekiuka pakubwa haki za binadamu na kukandamiza matakwa ya wananchi na kuigeuza nchi hiyo kuwa gereza kubwa huku wafungwa wa kisiasa wanaoshikiliwa katika magereza mbalimbali wakikabiliwa na hali mbaya.
Bi Ebtisam Al-Saegh, mwanaharakati na mtetezi wa haki za binadamu nchini Bahrain anazungumzia jambo hilo kwa kutoa ushahidi uliopo unaoonyesha juu ya kuzuiwa wafungwa wa kisiasa wagonjwa kupelekwa hospitali na kuandika: Kuhusiana na suala la afya na uzima wa wafungwa wa kisiasa kumekuwa kukifanyika upuuzaji wa makusudi, na jambo hilo limepelekea kuongezeka idadi ya wafungwa wa kisiasa wanaougua maradhi hatari.
T
Tangu Februari 14 mwaka 2011 hadi sasa, Bahrain imekuwa uwanja wa maandamano ya amani ya wananchi wanaoupinga utawala wa kiukoo wa Aal Khalifa. Wananchi hao wanataka kuwepo uhuru, utekelezwe uadilifu, ukomeshwe ubaguzi na kuundwa serikali itakayochaguliwa na wananchi wenyewe. Hali ya haki za binadamu nchini Bahrain inazidi kuwa mbaya siku baada ya siku na filihali hali hiyo imefikia kiwango kibaya na hatari mno. Kwa hakika utawala wa Aal Khalifa wa Bahrain una faili jeusi na la kutisha katika uga wa haki za binadamu.
Baraza la Haki za Binadamu na asasi zote za kimataifa zimekuwa zikitoa nyaraka na ushahidi unaoonyesha kwamba, utawala huo umekuwa ukiua raia wake, ukiwalazimisha wawe wakimbizi na ukiwa na lengo la kuvuruga muundo wa kijamii wa nchi hiyo umekuwa ukiwapatia uraia watu wa mataifa mengine. Kwa hali inavyoonekana hivi sasa, hakuna matumaini ya utawala huo kubadilisha mwenendo wake huo dhidi ya raia wa nchi hiyo, kwani mbinu za mfumo unaotawala nchini humo ni udikteta, ukandamizaji, mauaji na kuwafunga jela wapinzani.
Kubakia madarakani kwa utawala wa kifamilia nchini Bahrain kunafungamana na sababu kuu mbili. Mosi, misaada ya kifedha na kijeshi ya Saudi Arabia na Imarati na pili ni uungaji mkono wa kisiasa na kisilaha wa Marekani na Uingereza pamoja na nchi nyingine za Ulaya. Hapana shaka kuwa, usingekuwa uingiliaji wa Saudi Arabia na Imarati katika kuuunga mkono utawala wa Aal Khalifa nchini Bahrain, utawala huo usingekuwa na ubavu wa kukabiliana na mapambano ya wananchi.
Kiujumla ni kuwa, hali ya wafungwa katika magereza ya Bahrain ni mbaya mno na wafungwa wa kisiasa wamekuwa wakishinikizwa zaidi huku wakinyimwa haki za kimsingi kama za matibabu na kutembelewa na familia zao. Magereza ya Bahrain yanahesabiwa kuwa jela zenye msongamano mkubwa zaidi ulimwenguni na kuna wanaharakati wa masuala ya kibinadamu na wanasiasa wengi ambao wanashikiliwa katika magereza hayo.
Mwenendo wa kuwakandamiza raia nchini Bahrain ambao unafanyika chini ya uungaji mkono wa madola ya Magharibi na kimya cha jamii ya kimataifa, umeufanya utawala wa Aal Khalifa wa nchi hiyo uweke rekodi mpya katika uwanja wa kukiuka haki za binadamu.
Tukitupia jicho utendaji pamoja na takwimu mbalimbali kuhusiana na jinai za utawala wa Aal Khalifa tunaona kuwa, utawala huo haujaacha kutenda jinai ya aina yoyote ile katika hatua zake za kuwakandamiza raia. Hapana shaka kuwa, hatua hizo za viongozi wa Bahrain zinazidi kuweka wazi utambulisho halisi wa utawala wao ambao umejengeka juu ya misingi ya udikteta.
Siasa zilizo dhidi ya ubinadamu za utawala wa Aal Khalifa za kuwapokonya raia wa nchi hiyo haki zao zimeifanya nchi hiyo itambuliwe kuwa, moja kati ya wakiukaji wakuu wa haki za binadamu duniani.