Jeshi la Israel: Kuuawa Nasrullah kutatoa pigo kubwa kwa Hizbullah
Kamanda wa ngazi za juu wa utawala wa Kizayuni wa Israel ametoa mwito wa kuuawa Katibu Mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon, Sayyid Hassan Nasrullah akisisitiza kuwa, kuuawa kwake kutatoa pigo kubwa kwa harakati hiyo ya muqawama.
Katika makala iliyochapishwa kwenye jarida la Ma'arakhot linaloandikwa kwa lugha ya Kiebrania, Kanali Roy Levy, Kamanda Mkuu wa Kikosi cha 300 cha jeshi la utawala wa haramu wa Israel amesema Nasrullah anapaswa kuuawa katika operesheni ya makomandoo na jeshi la anga la utawala huo khabithi.
Kamanda huyo wa jeshi katili la Israel ameandika kuwa: Shakshia na tajriba yake (Nasrullah) jeshini imemfanya awe kitovu kikuu na kiongozi mwenye athari kubwa miongoni mwa makamanda wa ngazi za juu na hata askari wa ngazi za chini wa harakati yake. Kulengwa kwake kutafifiza moyo wa kupigana wa maadui.
Mapema mwezi huu, Sayyid Nasrullah alisisitiza kuwa, damu ya mashahidi na mhimili wa dhahabu wa jeshi, wanachi na muqawama umemfanya adui Mzayuni asithubutu kuishambulia kijeshi Lebanon.
Hii sio mara ya kwanza kwa Wazayuni kutoa matamshi ya kijuba ya kutishia kuwaua viongozi wa harakati za muqawama.
Wiki iliyopita, Yoav Galant, Waziri wa Ujenzi wa Vitongoji haramu wa utawala wa Kizayuni wa Israel alitoa vitisho vya kuuawa kigaidi Yahya Sinwar, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS katika Ukanda wa Gaza.