Walowezi wa Kizayuni wavamia tena Msikiti Mtakatifu wa al-Aqswa
(last modified Fri, 11 Jan 2019 04:13:23 GMT )
Jan 11, 2019 04:13 UTC
  • Walowezi wa Kizayuni wavamia tena Msikiti Mtakatifu wa al-Aqswa

Makumi ya walowezi wa Kizayuni wamevamia tena Msikiti wa al-Aqswa wakisaidiwa na askari wa jeshi la utawala haramu wa Israel na kufanya vitendo vya kuuvunjia heshima msikiti huo mtakatifu na kibla cha kwanza cha Waislamu.

Habari kutoka Palestina zinasema kuwa, jana walowezi wa Kizayuni waliuvamia msikiti wa al-Aqswa kupitia Babul al-Maghariba ambapo baada ya kuingia katika msikiti huo walifanya mambo ya kichochezi.

Hujuma na uvamizi wa walowezi wa Kizayuni katika Msikiti wa al-Aqswa umeongezeka mno katika siku za hivi karibuni. 

Inaelezwa kuwa, karibu kila siku walowezi wa Kizayuni wamekuwa wakifanya uvamizi katika msikiti huo lengo likiwa ni kutekeleza njama za kutokomeza utambulisho wa Kiislamu na Kikristo wa Msikiti wa al-Aqswa na badala yake kuweka nembo za Kizayuni.

Walowezi wa Kizayuni walipovamia Msikiti wa al-Aqswa

Katika miaka ya hivi karibuni, utawala wa Kizayuni wa Israel umeshadidisha hujuma na uvamizi wake dhidi ya maeneo ya Wapalestina ukifanya juhudi za kufikia malengo yake haramu katika ardhi za Wapalestina.

Hata hivyo kusimama kidete wananchi wa Palestina hadi sasa kumekwamisha njama na mipango yote ya Wazayuni, zikiwemo njama zake za kubadilisha muundo wa kijamii na kijiografia wa Baytul Muqaddas. 

Abdul Adhim Salhab, Mkuu wa Baraza la Waqfu za Kiislamu katika mji wa Quds ametangaza kuwa, zaidi ya walowezi wa Kizayuni 30,000 waliingia kinyume cha sheria katika msikiti wa al-Aqswa katika mwaka uliomalizika wa 2018 na kwamba, idadi hiyo ni ongezeko la asilimia 17 ikilinganishwa na mwaka wa kabla yake.