Sayyid Hassan Nasrullah: Uimara wa muqawama umesambaratisha njama zote za Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i52042-sayyid_hassan_nasrullah_uimara_wa_muqawama_umesambaratisha_njama_zote_za_marekani
Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon Sayyid Hassan Nasrullah amesema kuwa, Marekani ilikuwa na njama kubwa tofauti kwa ajili ya kuhitimisha muqawama mwaka 2006, lakini uimara wa muqawama ukafanikisha kusambaratisha njama zote hizo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 09, 2019 01:16 UTC
  • Sayyid Hassan Nasrullah: Uimara wa muqawama umesambaratisha njama zote za Marekani

Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon Sayyid Hassan Nasrullah amesema kuwa, Marekani ilikuwa na njama kubwa tofauti kwa ajili ya kuhitimisha muqawama mwaka 2006, lakini uimara wa muqawama ukafanikisha kusambaratisha njama zote hizo.

Sayyid Hassan Nasrullah aliyasema hayo Ijumaa ya jana katika hotuba aliyoitoa kwa mnasaba wa kumbukumbu ya mwaka wa 31 wa kuasisiwa kamati ya uungaji mkono kwa muqawama wa Kiislamu ambapo sambamba na kuashiria suala la vikwazo vya Uingereza na hatua ya London ya kuiweka Harakati ya Hizbullah katika orodha ya makundi ya kigaidi amesema kuwa, tangu mwaka 2011 kulianza njama chafu kwa ajili ya kutoa pigo kwa muqawama. Ameongeza kwamba kuwarejesha nchini Iraq wanachama wa kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS) na pia kuendeleza mashinikizo dhidi ya Lebanon, Palestina na Yemen, ni miongoni mwa njama hizo. Sayyid Hassan Nasrullah amebainisha kwamba hatua ya kuuwekea vikwazo muqawama haitokani na udhaifu wa harakati hiyo, bali inatokana na uwezo mkubwa wa muqawama na kuongeza kwamba, hatua zote hizo chafu ziliratibiwa na Marekani na utawala haramu wa Kizayuni pamoja na nchi za eneo la magharibi mwa Asia.

Marekani na Israel ambazo baada ya kushindwa kupambana na Hizbullah zimebakia kutumia silaha ya vikwazo

Akibainisha kwamba huenda pia vikwazo vya Marekani vikashadidishwa dhidi ya mrengo wa muqawama, amesema kwamba, hii ni kwa sababu muqawama umeweza kusambaratisha ajenda chafu za Washington na utawala wa Kizayuni na ambazo zimekuwa zikiungwa mkono na pande kadhaa katika eneo. Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon amebainisha kwamba kama ambavyo muqawama ulivyosimama imara katika kukabiliana na njama za Rais Donald Trump wa Marekani kwa ajili ya kufanikisha ajenda yake kupitia mradi wa 'Muamala wa Karne', amesema kuwa, sababu kuu ya kuiweka harakati ya Hizbullah katika orodha ya makundi ya kigaidi, inatokana na kushindwa Marekani na washirika wake katika kukabiliana na harakati hiyo ambayo kila siku inazidi kuwa na nguvu, irada na uimara wa hali ya juu. Amesisitiza kwamba nchini Lebanon muqawama huo hauungwi mkono tu na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, bali na Walebanon wote ambao wamekuwa wakitoa misaada mingi kwa harakati hiyo.