Syria: Marekani ndio tishio la usalama na amani ya kimataifa
Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria sambamba na kulaani vikali matamshi ya Rais Donald Trump wa Marekani kuhusiana na miinuko ya Golan inayokaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Israel, imesema kuwa siasa za kupenda kujitanua na za mabavu za Washington, ndio sababu kuu ya kuibuka ghasia na tishio kwa usalama na uthabiti wa kimataifa.
Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria jana Ijumaa imesema kuwa, kwa mara nyingine matamshi ya Trump yamebainisha upendeleo wa kibubusa wa Marekani kwa utawala haramu wa Kizayuni. Imezidi kufafanua kwamba uamuzi wa rais huyo wa Marekani ni ukiukaji wa wazi wa azimio nambari 497 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na imeongeza kwamba Washington imeamua kuifanyia maskhara jamii ya kimataifa na maazimio yake. Inafaa kuashiria kuwa, azimio nambari 497 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililopitishwa mwaka 1981 ambapo akthari ya wajumbe wa baraza hilo ikiwemo Marekani yenyewe, waliyatangaza maamuzi ya utawala wa Kizayuni na hatua zake kuihusu miinuko ya Golan kuwa batili, huku wakipinga vikali kuiunganisha miinuko hiyo na ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu (Israel).
Katika fremu hiyo Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria imebainisha kwamba miinuko ya Golan ni eneo la Kiarabu ambalo ni mali halali ya Syria na imesisitiza kwamba raia wa Syria wanayo azma thabiti kwa ajili ya kulirejesha eneo hilo kwenye ardhi ya nchi hiyo ya Kiarabu. Alkhamisi ya jana Trump aliandika ujumbe wa kichochezi kwenye mtandao wa Twitter kwamba, baada ya kupita miaka 52 wakati umefika kwa Marekani kutambua rasmi umiliki wa Israel kwa miinuko ya Golan inayokaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni.