Kuwait yasusia mkutano wa Bahrain kutokana na kushiriki Wazayuni
Kufuatia ushiriki wa idadi kadhaa ya viongozi wa Kizayuni katika mkutano uliopewa jina la 'Ujasiriamali' nchini Bahrain, Waziri wa Viwanda wa Kuwait ametangaza kususia mkutano huo.
Gazeti la Al-Quds Al-Arabi limemnukuu Abdullah Al-Kandari, mwakilishi wa bunge nchini Kuwait akisema kuwa, Waziri wa Viwanda wa nchi hiyo, Khaled Al-Rawdan amelazimika kususia mkutano huo. Al-Kandari ameongeza kwamba, Al-Rawdan amechukua uamuzi huo kutokana na ombi la bunge la nchi hiyo ambalo limemtaka asishiriki mkutano huo utakaofanyika katikati ya mwezi huu wa Aprili nchini Bahrain.
Mwakilishi huyo wa bunge nchini Kuwait ameashiria msimamo wa taifa la Kuwait wa kupinga kitendo cha baadhi ya watawala wa Kiarabu cha kuboresha mahusiano na utawala wa Kizayuni kupitia kongamano hilo la Ujasiriamali nchini Bahrain kuwa ni kinyume kabisa na misimamo ya Kuwait. Aidha wabunge wa Kuwait wamezitaka nchi nyingine kususia kongamano hilo la mjini Manama na wametangaza kwamba ushiriki wake una maana ya kuboresha uhusiano na utawala khabithi wa Kizayuni unaoukalia kwa mabavu mji wa Quds, kilipo kibla cha kwanza cha Waislamu duniani.