Zarif: Migogoro ya eneo inatokana na sera za Marekani
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema migogoro ya Asia Magharibi inatokana na sera za Marekani zenye malengo ya muda mfupi, maamuzi ya upande mmoja na uhasama wa utawala wa sasa wa Marekani.
Mohammad Javad Zarif ameyasema hayo leo Jumatano mjini Doha katika kongamano la "Jukwaa la Mazungumo ya Ushirikiano Asia" na kuongeza kuwa wakati dola lenye nguvu linalilazimisha taifa lingine kufuata matakwa yake, hatua hiyo ni sawa na tishio kwa wote. Ameongeza kuwa: "Maadamu nchi hazitumii uwezo wao kwa ajili ya kudhamini msingi wa maamuzi ya pande kadhaa, sera za maamuzi ya upande mmoja zitajikita na baada ya hapo utawala wa msituni utachukua mahala pa utawala wa sheria."
Zarif aidha amesisitiza kuhusu utatuzi wa matatizo ya kieneo kupitia mazungumzo na kuongeza kuwa: "Iran imeshatoa pendekezo la kuundwa 'Jukwaa la Mazungumzo ya Kieneo katika Ghuba ya Uajemi."

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu inaunga mkono mazungumzo na sera za pande kadhaa. Aidha amesema ili Jukwaa la Mazungumo ya Ushirikiano Asia liwe athirifu, linapaswa kuwa na makao makuu yenye uwezo wa kitaalamu wa utendaji.
Jukwaa la Mazungumo ya Ushirikiano Asia lilianzishwa Japan mwaka 2002 kwa lengo la kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na kuandaa mazingira ya amani endelevu kupitia mazungumzo ya kieneo. Jukwaa hilo lina nchi wanachama 34.