Saudia na Imarati kushiriki mkutano wa Marekani dhidi ya Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i53650-saudia_na_imarati_kushiriki_mkutano_wa_marekani_dhidi_ya_palestina
Tawala vibaraka za Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu zimetangaza kuwa zitashiriki mkutano wa Marekani wa kuzindua hatua ya mwanzo ya utekelezaji wa 'Muamala wa Karne' mwezi ujao wa Juni nchini Bahrain.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 22, 2019 21:58 UTC
  • Saudia na Imarati kushiriki mkutano wa Marekani dhidi ya Palestina

Tawala vibaraka za Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu zimetangaza kuwa zitashiriki mkutano wa Marekani wa kuzindua hatua ya mwanzo ya utekelezaji wa 'Muamala wa Karne' mwezi ujao wa Juni nchini Bahrain.

Shirika rasmi la habari la Saudia SPA liliripoti jana Jumatano kuwa, Riyadh itatuma ujumbe wa ngazi ya juu utakaoongozwa na Waziri wa Uchumi na Mipango wa nchi hiyo ya kifalme kwenda kushiriki mkutano huo wenye anwani bandia ya "Amani na Ufanisi" kwa Wapalestina wa Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Aidha Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ya Umoja wa Falme za Kiarabu imesema Abu Dhabi itatuma ujumbe kwenye mkutano huo wa Manama. 

Hii ni katika hali ambayo, Harakati ya Jihad Islami ya Palestina, Harakati ya Ukombozi wa Palestina PLO na Harakati ya Muqawama wa Kiislamu wa Palestina (HAMAS) katika nyakati tofauti zimepinga vikali mpango huo wa Marekani wa "Muamala wa Karne" zikisisitiza kuwa kuuunga mkono ni sawa na kuwasiliti wananchi madhulumu wa Palestina.

Wapalestina wakiandamana kupinga Muamala wa Karne

Wapalestina wamekuwa wakiulaani na kuupinga vikali mpango huo wa 'Muamala wa Karne' wakiutaja kuwa ni moja ya njama kubwa zaidi dhidi ya taifa madhulumu la Palestina linalokaliwa kwa mabavu na utawala ghasibu wa Israel.

Mkwe wa Rais Donald Trump wa Marekani, Jared Kushner hivi karibuni alifichua kuwa, hatua ya kwanza ya 'Muamala wa Karne' itazinduliwa na Marekani nchini Bahrain katika 'Kongamano la Kiuchumi' litakalofanyika Juni 25 na 26.