Baada ya kutupwa mkono na Marekani, sasa Wakurdi wa Syria wajiandaa kujiunga na serikali
(last modified Wed, 09 Oct 2019 02:32:58 GMT )
Oct 09, 2019 02:32 UTC
  • Baada ya kutupwa mkono na Marekani, sasa Wakurdi wa Syria wajiandaa kujiunga na serikali

Kamanda Mkuu wa Wanamgambo wa Kikurdi nchini Syria ameelezea uwezekano wa kushirikiana na serikali ya Damascus kwa ajili ya kukabiliana na mashambulizi ya Uturuki dhidi ya maeneo ya mpakani kaskazini mwa Syria.

Mazlum Abdi ambaye ni kiongozi wa wanamgambo wa kundi la Wapiganaji wa Kidemokrasia waliokuwa wakiungwa mkono na Marekani amesema kuwa, moja ya machaguo ya wapiganaji walio chini ya kundi hilo kwa ajili ya kujitetea kutokana na mashambulizi ya Uturuki ni kushirikiana na Rais Bashar al-Assad wa Syria.

Hatua hiyo ya wanamgambo wa Kikurdi nchini Syria imechukuliwa baada ya serikali ya Marekani siku ya Jumatatu kutoa taarifa inayohusu kurejea nyuma askari wa nchi hiyo kutoka baadhi ya ngome za kijeshi kaskazini mwa Syria.

Mazlum Abdi, kiongozi wa wanamgambo wanaoitwa 'Wapiganaji wa Kidemokrasia'

Katika hatua nyingine, makumi ya watu wa jamii ya Wakurdi nchini Syria katika maeneo ya mpakani ya Qamishli, Sari Kani na Tell Abiad wamefanya maandamano kulalamikia hatua za Uturuki ya kuanzisha mashambulizi mashariki mwa Mto Furati. Duru za maeneo hayo zimeripoti kuwa, jeshi la Uturuki limeanza kushambulia ngome na vituo vya kundi la People's Protection Units (YPG) la Wakurdi wa Syria katika mji wa al-Malikiyah ambalo serikali ya Ankara inadai lina mfungamano na magaidi wa kundi la PKK.

Tags