Bashar Assad: Syria itajibu kisheria mashambulizi ya Uturuki
Rais Bashar al Assad wa Syria amesema hadi sasa nchi yake imeshatoa jibu kwa mashambulizi ya Uturuki na magaidi waitifaki wa Uturuki na kuongeza kuwa Syria itatumia uwezo wake wote wa kisheria kujibu mashambulizi dhidi yake.
Rais Assad ameyasema hayo Alhamisi mjini Damascus alipokutana na kufanya mazungumzo na Falih al-Fayyadh Mshauri wa Usalama wa Taifa la Iraq ambaye amemkabidhi rais wa Syria barua kutoka kwa Waziri Mkuu wa Iraq Adel Abdul Mahdi.
Katika barua yake, Waziri Mkuu wa Syria ameashiria masuala kama vile uimarishwaji uhusiano wa pande mbili, mapambano dhidi ya ugaidi, usalama wa mipaka na matukio ya hivi karibuni.
Katika kikao hicho, Bashar Assad amesisitiza kuwa: "Madola ajinabi yanalitazama eneo la Asia Magharibi kwa tamaa na hujuma ya kijinai ya Uturuki dhidi ya Syria inaweza kutathminiwa katika fremu hiyo." Assad amesema Uturuki imetumia nara bandia kutetea mashambulizi yake dhidi ya Syria.
Kwa upande wake, Falih al-Fayyadh Mshauri wa Usalama wa Taifa Iraq amesisitiza kuhusu ushirikiano wa nchi mbili ili kufikia maslahi ya pamoja ya kitaifa na kuimarisha usalama wa nchi mbili.
Mshauri wa Usalama wa Taifa nchini Iraq ameitembelea Syria wakati ambao kuanzia 9 Oktoba Uturuki ilianzisha hujuma ya kijeshi dhidi ya eneo la kaskazini mwa Syria.
Serikali ya Syria imeitaja oparesheni hiyo ya kijeshi kuwa ni uvamizi na ukaliaji mabavu nchi yake na kwamba itakabiliana na hujuma hiyo.