Putin atembelea Syria na kukutana Assad, atembelea mitaa ya Damascus
(last modified Wed, 08 Jan 2020 02:49:24 GMT )
Jan 08, 2020 02:49 UTC
  • Putin atembelea Syria na kukutana Assad, atembelea mitaa ya Damascus

Rais Vladimir Putin wa Russia jana aliwasili Damascus mji mkuu wa Syria na kukutana na Rais wa nchi hiyo, Bashar Assad.

Taarifa iliyotolewa na ikulu ya Rais wa Russia, Kremlin imesema marais hao wawili wamebadilishana mawazo juu ya hali ya sasa ya Syria na jinsi ya kulinda umoja wa ardhi ya nchi hiyo. Imesema Rais Putin ameeleza kuridhishwa kwake na kazi iliyofanyika ya kurejesha hali ya kawaida katika mitaa ya mji mkuu wa Syria, Damascus. Putin amesema Syria imepiga hatua na kuvuka visingiti vikubwa katika njia ya kuimarisha mamlaka ya serikali halali ya nchi hiyo

Kwa upande wake Rais Bashar Assad wa Syria amemshukuru mgeni wake wa Russia kwa misaada ya nchi hiyo katika mapambano dhidi ya ugaidi.

Hii ni safari ya kwanza kufanywa na Rais Vladimir Putin wa Russia nchini Syria baada ya safari yake nchini humo mwaka 2017 wakati alipotembelea Kambi ya Jeshi la Anga la Russia ya Hmeymim katika mkoa wa Latakia.

Wakati huo huo habari zinasema manuwari ya kivita ya kurusha makombora ya Russia, Marshal Ustinov, imevuka malango bahari ya Bosphorus na Dardanelles na kuingia katika Bahari ya Mediterania.

Marshal Ustinov

Shirika la habari la Sputnik limeripoti kuwa manuwari hiyo ya kivita imetumwa katika neo hilo ghafla kutokana na hali ya mivutano inayoendelea katika eneo la magharibi mwa Asia baada ya Marekani kumuua kigaidi Jenerali Qassem Soleimani kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran (Sepah).