Syria yalaani hatua ya Marekani kutuma askari zaidi nchini humo
(last modified 2016-04-29T04:08:24+00:00 )
Apr 29, 2016 04:08 UTC
  • Syria yalaani hatua ya Marekani kutuma askari zaidi nchini humo

Serikali ya Syria imekosoa vikali hatua ya Marekani kutuma askari zaidi nchini humo na kutaja hatua hiyo kama uvamizi dhidi ya uhuru wa kujitawala wa nchi hiyo ya Kiarabu.

Taarifa ya Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Syria imesema kuwa, serikali ya Damascus imeichukulia kwa uzito habari ya kuwasili askari 150 wa Marekani katika eneo la Rumeilan, mashariki mwa nchi bila ya idhini ya serikali. Taarifa hiyo imesema hatua hiyo ni ya kichokozi na kivamizi na isiyokubalika hata kidogo. Taairifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria imeongeza kuwa, kutumwa askari wa kigeni katika ardhi ya nchi hiyo bila kibali wala kuishauri serikali husika ni dharau, kutoheshimu uhuru wa kujitawala na ukiukaji wa sheria za kimataifa.

Siku ya Jumatano, Russia ilifichua kuwa, tayari kikosi cha kwanza cha askari 150 wa Marekani kimewasili Syria kupitia uwanja wa ndege wa kijeshi wa Rumeilan katika mkoa wa Hasakah, mashariki mwa nchi.

Siku ya Jumanne, Rais Barack Obama wa Marekani akiongea mjini Hannover nchini Ujerumani alisema Washington katika kipindi cha wiki kadhaa zijazo itatuma askari 250 zaidi wa nchi kavu kuungana na Vikosi vya Operesheni Maalumu vya Marekani eti kwa lengo la kukabiliana na kundi la kigaidi la ISIL. Maria Zakharova, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Russia alisema kuwa Moscow inafuatilia kwa karibu hatua ya Marekani kutuma vikosi zaidi nchini Syria.

Karibu watu laki 5 wameuawa nchini Syria tangu Machi mwaka 2011, kutokana na vita vilivyoanzishwa na makundi ya kigaidi yanayoungwa mkono na madola ya Magharibi na hasa Marekani pamoja na waitifaki wake wa eneo kwa lengo la kuiondoa madarakani serikali halali ya nchi hiyo.

Tags