Malengo ya safari ya Macron mjini Beirut
Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa amefanya safari katika mji mkuu wa Lebanon, Beirut, siku mbili tu baada ya kutokea mlipuko mkubwa uliosababisha maafa na hasara kubwa katika mji huo.
Amekuwa kiongozi wa kwanza wa Magharibi kuitembelea Lebanon mara tu baada ya kutokea mlipuko huo wa kutisha uliosababisha maafa na uharibifu mkubwa hapo siku ya Jumanne. Aliwasili katika mji huo wa bandari na ndege tatu zilizokuwa zimesheheni madawa na bidhaa nyingine za kibinadamu kwa madai ya kuwasaidia watu walioathirika kutokana na mkasa huo.
Mlipuko huo wa Jumanne ulisababisha hasara kubwa katika bandari ya Beirut ambacho ndicho kituo muhimu zaidi kinachotumika kusafirisha nje na kuingiza ndani ya nchi bidhaa zinazoagizwa na Lebaon kutoka nchi za kigeni. Bila shaka mlipuko huo utatoa pigo kubwa la kiuchumi na kisiasa kwa Lebanon ambayo kabla ya hapo tayari ilikuwa inakabiliwa na mgogoro mkubwa wa kiuchumi na kisiasa.
Safari ya Macron huko Lebanon bila shaka imekuwa ikifuatilia malengo mengine ya siri yaliyo nje ya mipaka ya misaada ya kibinadamu.
Lebanon ilikuwa kolono la Ufaransa na bado nchi hiyo ya Magharibi inafuatilia malengo ya kisiasa nchini humo na katika eneo zima la Asia Magharibi. Hali ya kisiasa inayotawala sasa nchini Lebanon inatokana na siasa za kikoloni za Ufaransa.
Ufaransa ikiwa mshirika muhimu wa utawala ghasibu wa Israel imekuwa ikifuatilia siasa za kuyadhoofisha makundi ya Kiislamu katika nchi hiyo ya Kiarabu. Wiki mbili zilizopita Jean-Yves Le Drian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa aliitembelea nchi hiyo kwa ajili ya kufuatilia maslahi ya kisiasa ya Ufaransa.
Alisema katika safari hiyo kwamba sharti la Lebanon kupewa mkono na Mfuko wa Fedha wa Kimataifa IMF ni kufanyika marekebisha muhimu ya kisiasa nchini humo. Sehemu ya sharti hilo ni kupunguzwa ushawishi wa chama cha Hizbullah katika mfumo wa utawala wa Lebanon. Hizbullah inahesabika kuwa ngome imara na kizuizi muhimu mkabala na siasa za kichokozi za utawala haramu wa Israel nchini Lebaon na katika eneo zima la Asia Magharibi.
Hizbullah bila shaka iko mstari wa mbele katika muhimili wa mapambano ya Kiislamu dhidi ya siasa za kieneo za Marekani na nchi za Ulaya zikiongozwa na Ufaransa. Katika kipindi cha muongo mmoja uliopita, Ufaransa na nchi nyinginbe za Ulaya zimetumia uwezo wao wote kwa ajili ya kutoa pigo dhidi ya muhimili huo na hasa Hizbullah, lakini bila ya mafanikio makubwa.
Siasa za nchi za Magharibi za kuibua migogoro nchini Syria tokea mwaka 2011 na kuyaunga mkono kwa hali na mali makundi ya kigaidi na kitakfiri yanayopigana dhidi ya serikali halali ya nchi hiyo zimekuwa zikitekelezwa kwa lengo hilo hilo. Pamoja na hayo yote lakini siasa hizo hazijafanikiwa pakubwa. Ufaransa na washirika wake wa Ulaya kwa kuliweka jina la Hizbullah katika orodha ya makundi yanayodaiwa kuwa ya kigaidi, zinajaribu kuishinikiza serikali ya Lebanon na nchi nyingine zinazounga mkono mrengo wa mapambano ya Kiislamu, zisitishe uungaji mkono huo kwa Hizbullah.
Matukio ya karibuni huko Beirut yameiweka serikali ya Lebanon katika hali ngumu kisiasa na kiuchumi. Kufikia sasa serikali za nchi za Magharibi zimethibitisha wazi kwamba suala la haki za binadamu huwa na umuhimu kwao pale tu zinapoweza kulitumia kwa ajili ya kudhamini maslahi yao ya kisiasa katika mataifa tofauti ya dunia.
Hivi sasa serikali ya Lebabon inahitajia mkopo wa IMF kuliko wakati mwingine wowote. Idhini ya Ufaransa na Marekani ya kutolewa mkopo huo bila shaka itarahisisha njia ya kutolewa mkopo huo. Kabla ya hapo nchi mbili hizo za Magharibi zilikuwa zimeshurutisha kutolewa mkopo huo na kupunguzwa ushawishi wa Hizbullah katika serikali ya Lebanon.
Adnan Mansur, Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Lebanon katika mahojiano yake na kanali ya habari ya al-Aalam wiki mbili zilizopita kuhusiana na safari ya Jean-Yves Le Drian nchini Lebanon, alisema kwamba Ufaransa na Umoja wa Ulaya haziwezi kutekeleza siasa zao nje ya mashinikizo na ushawishi wa Marekani, bali siasa zao zote zinaakisi moja kwa moja siasa za Marekani.
Aliashiria mashinikizo ya Marekani na mzingiro wa nchi hiyo dhidi ya Lebanon na kuongeza kuwa Sheria ya Caesar imeharibu zaidi hali ya mambo nchini humo. Alisema sheria hiyo haiilengi Syria tu bali inailenga nchi yoyote inayokusudia kudumisha ushirikiano wake na serikali ya Damascus. Alisisitiza kuwa kwa sasa Lebanon ikiwa jirani mwema wa Syria ndiyo inayodhurika zaidi na sheria hiyo ya kibeberu.