Uenyekiti wa Arab League wageuka kiazi moto, Libya pia yaukataa
Siku chache baada ya Qatar na Kuwait kukataa kuchukua uenyekiti wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) badala ya Palestina ambayo nayo ilikataa uenyekiti huo, Libya pia imeamua kufuata mkumbo huo.
Bila ya kutoa maelezo ya kina, Serikali ya Muafaka wa Kitaifa ya Libya ilitangaza Jumanne ya jana katika taarifa kuwa, haitochukua urais wa Arab League.
Nchi hizo za Kiarabu zimekataa kubeba jukumu hilo kama zinavyotakiwa kufanya na Kipengee cha Sita cha Kanuni za Arab League.
Hatua ya nchi ya tatu katika Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ya kukataa kuchukua uenyekiti wa kiduru wa jumuiya hiyo inatahminiwa na wachambuzi wa mambo kuwa pigo kubwa kwa Arab League na ishara ya wazi ya kuweko upinzani mkali dhidi ya mkumbo wa baadhi ya mataifa ya Kiarabu wa kuanzisha uhusiano na utawala ghasibu wa Israel.
Jumanne ya Septemba 22, Mamlaka ya Ndani ya Palestina ilitangaza kusamehe haki yake ya kuchukua uenyekiti wa Arab League lakini ikasisitiza kuwa itaendelea kuwa mwanachama wa jumuiya hiyo.
Ilisema itaendelea kuwa mwanachama licha ya hatua ya baadhi ya nchi za Kiarabu ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel na kusisitiza kuwa kama itajitoa kutazidi kuzuka pengo katika ulimwengu wa Kiarabu.