Saudi Arabia yaruhusu Umra kwa mahujaji wa kigeni
Serikali ya Saudi Arabia imewaruhusu mahujaji kutoka nje kuingia nchini humo kwa ajili ya kutekeleza ibada ya Umra baada ya kufungwa mwezi Machi mwaka huu kutokana na maambukizi ya virusi vya corona.
Televisheni rasmi ya Saudi Arabia imetangaza kuwa, awamu ya tatu ya kuanza tena ibada ya Umra ilianza usiku wa Jumamosi ya jana na kwamba, mahujaji wa ndani na nje ya nchi wameruhusiwa kufanya ibada ya Umra, ziara na Swala ndani ya Msikiti wa Makka.
Awamu hiyo ya tatu inaruhusu kuanza hatua kwa hatua ibada ya Umra ya watu elfu 20, na watu elfu 60 kutekeleza ibada ya Swala kila siku ndani ya Masjidul Haram, sambamba na kulinda sheria za kukabiliana na virusi vya corona.
Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Hija na Umra ya Saudia ilitangaza jana kwamba kundi la kwanza na Mahujaji kutoka nje ya Saudi Arabia litawasili nchini humo leo Jumapili.
Jumamosi ya jana pekee Saudi Arabia ilisajili kesi 402 za maambukizi ya virusi vya corona na 19 miongoni mwao waliaga dunia.
Hadi sasa watu 5,402 wameaga dunia nchini Saudi Arabia kutokana na virusi vya corona.