Mripuko wa ugonjwa wa kipindupindu waua 50 nchini Nigeria
Makumi ya watu wameripotiwa kuaga dunia kutokana na mripuko wa maradhi ya kipindupindu nchini Nigeria.
Taarifa iliyotolewa jana Jumanne na Kituo cha Kudhibiti Magonjwa cha Nigeria (NCDC) imesema kwamba, kesi za ugonjwa huo zilizorekodiwa kufikia sasa ni 1,746, vikiwemo vifo 50.
Chikwe Ihekweazu, Mkuu wa NCDC amesema kesi zinazoshukiwa kuwa za ugonjwa wa kipindupindu zimenakiliwa katika majimbo ya Nasarawa, Sokoto, Kogi, Bayelsa, Gombe, Zamfara, Delta na Benue.
Afisa huyo wa afya wa Nigeria amesema wamechukua hatua faafu kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo katika maeneo mengine ya nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.
Ugonjwa wa kipindupindu husababishwa na bakteria aina ya Vibrio Cholera na huenezwa kwa kunywa maji yasiyo salama. Dalili za ugonjwa huo ni maumivu ya tumbo, kuharisha, kutapika pamoja na homa.
Miripuko ya maradhi hayo hatarishi huripotiwa nchini Nigeria mara kwa mara, hususan katika misimu ya mvua za masika zinazoambatana na mafuriko.