Utawala wa Kizayuni wabomoa kikamilifu misikiti mitatu Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i70310-utawala_wa_kizayuni_wabomoa_kikamilifu_misikiti_mitatu_gaza
Utawala wa Kizayuni wa Israel mbali na kufanya mauaji dhidi ya Wapalestina katika hujuma na mashambulio yake ya kinyama yanayoendelea, umebomoa kikamilifu misikiti mitatu katika Ukanda wa Gaza.
(last modified 2026-02-05T09:20:29+00:00 )
May 19, 2021 06:53 UTC
  • Utawala wa Kizayuni wabomoa kikamilifu misikiti mitatu Gaza

Utawala wa Kizayuni wa Israel mbali na kufanya mauaji dhidi ya Wapalestina katika hujuma na mashambulio yake ya kinyama yanayoendelea, umebomoa kikamilifu misikiti mitatu katika Ukanda wa Gaza.

Wizara ya Waqfu wa Palestina imetangaza leo kuwa, misikiti mitatu huko katika Ukanda wa Gaza imebomolewa kikamilifu kufuatia hujuma na mashambulio ya anga ya jeshi vamizi la Israel.

Taarifa hiyo imeeleza pia kuwa, misikiti mingine 40 imedhurika na mashambulio hayo kutokana na baadhi ya sehemu zake kupigwa kwa makombora.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa zaidi ya raia 72,000 wamekuwa wakimbizi huko Gaza kutokana na mashambulio hayo mtawalia ya jeshi la Israel.

Jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel linaendeleza jinai zake dhidi ya Wapalestina huku jitihada za kimataifa za kuhakikisha usitishaji mapigano unatekelezwa zikiwa zimeshindwa na kugonga mwamba hadi sasa kutokana na ukwamishaji mambo unaofanywa na serikali ya Marekani.

Mashambulio ya anga ya Israel

 

Wakati huo huo, Riyadh al-Mansour, mwakilishi wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amesema kuwa, ni jambo la kuaibisha kuona Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeshindwa kuchukua msimamo wa kutaka mapigano yasimamishwe huko katika Ukanda wa Gaza.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, baadhi ya viongozi wa utawala haramu wa Israel wamenukuliwa wakikiri kwamba, utawala huo  haujawahi kushambuliwa kwa idadi kubwa ya makombora na makundi ya muqawama kama unavyoshambuliwa hivi sasa.