HAMAS: Hakuna dola lolote linaloweza kuwalazimisha Wapalestina watoke katika ardhi zao
Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amesisitiza kuwa, hakuna dola lolote duniani lenye uwezo wa kulilazisha taifa la Palesitna liondoke katika ardhi zake na kuzifumbia macho.
Hayo yameripotiwa leo Jumatano na shirika la habari la ISNA ambalo limemnukuu Ismail Hania akisema pia kuwa, makundi ya muqawama yamewatangazia wakazi wa eneo la Sheikh Jarrah huko Quds kwamba wanapaswa kusimama imara kulinda haki na ardhi yao.
Ameongeza kuwa, kadhia ya Palestina hailihusu taifa moja au umma mmoja tu, ndio maana njama za adui Mzayuni za kutaka kuwa na ushawishi na nguvu kubwa zaidi katika eneo hili kamwe hazitofanikiwa.
Mkuu huyo wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS vile vile amesema, makundi ya muqawama yanapaswa kuunda lobi moja madhubuti ya kukabiliana na lobi za Kizayuni huko Marekani na Ulaya kwani hatima ya yote, mapambano baina ya muqawama na utawala pandikizi wa Kizayuni yatakuwa ni kwa manufaa ya Palestina.
Katika kipindi cha karibuni, Wazayuni wamekuwa wakifanya njama kubwa za kuwalazimisha Wapalestina waondoke kwenye maeneo yao kama wale wa eneo la Sheikh Jarrah huko Quds, lakini Wapalestina wamesimama imara kulinda ardhi zao.