Nov 04, 2021 07:52 UTC
  • Sheikh Naeem Qasim
    Sheikh Naeem Qasim

Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah nchini Lebanon amesema kuwa uvamizi wa Marekani nchini Syria na juhudi za nchi hiyo za kutaka kuanzisha Mashariki ya Kati Mpya zimefeli na kugonga mwamba.

Sheikh Naeem Qasim amesema njama za Marekani za kutaka kuanzisha eneo eti la Mashariki ya Kati Mpya zimeshindwa na kwamba matukio yanayojiri sasa yanadhihirisha ushindi wa kambi ya muqawama na mapambano dhidi ya mabeberu na wazayuni. 

Naibu Katibu Mkuu wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon amesema Marekani inaendeleza hujuma na uvamizi dhidi ya Syria kwa kuendelea kuyafadhili makundi ya kigaidi yaliyoko katika kambi haramu ya Al-Tanf kwenye mpaka wa Syria na Jordan, kuiba mafuta ya nchi hiyo katika eneo la al Jazerah na kupitia vikwazo vya kiuchumi vya upande mmoja vya nchi za Magharibii dhidi ya watu wa Syria. Ameongeza kuwa, mashinikizo yote ya Marekani yameshindwa kuiondoa madarakani serikali ya Syria, bali kinyume chake, serikali hiyo imepata nguvu zaidi.

Wanajeshi wa Marekani wakiiba mafuta Syria

Sheikh Naeem Qasim amesema kuwa migogoro yote inayoshuhudiwa Syria, Lebanon na Palestina inatokana na maamuzi ya Marekani kwa ajili ya kuulinda utawala haramu wa Israel na kuuhalalisha utawala huo na kwamba vita vya Syria vimepelekea kufeli mradi huo. 

Tags