Oct 09, 2022 02:56 UTC
  • Damascus: Marekani inapaswa kuondoa mara moja majeshi yake kutoka Syria

Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria imesisitiza kuwa, Washington inapaswa kuondoa mara moja majeshi yake haramu katika ardhi ya Syria.

Jeshi la Marekani na makundi ya kigaidi yanayoshirikiana nalo limekuwepo kaskazini na mashariki mwa Syria kinyume cha sheria kwa muda mrefu, na mbali na kupora rasilimali za mafuta na nafaka za nchi hiyo, linachukua hatua dhidi ya wakazi na vikosi vya jeshi la Syria katika eneo hili.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria imetangaza kuwa Marekani inapaswa kuondoa mara moja majeshi yake haramu kutoka Syria na kuacha kuwaunga mkono magaidi, mamluki na wanamgambo wanaotaka kujitenga; makundi ambayo inayatumia kufikia malengo yake.

Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Syria imeongeza kuwa: Kuendelea siasa mbovu za Marekani za kuiba mafuta ya Syria kupitia mipaka ya Iraq na kuyahamishia kaskazini mwa nchi hiyo ni sawa na ujambazi na jitihada za kurejea katika zama za ukoloni.

Jeshi la Marekani linashirikiana na magaidi dhidi ya Syria

Taarifa hiyo imebainisha kuwa: Syria inakumbusha kwamba vitendo hivi vinakinzana na sheria za kimataifa na Mkataba wa Umoja wa Mataifa, na Damascus inaliomba Baraza la Usalama kulaani na kukomesha vitendo hivyo.

Imeelezwa katika taarifa hiyo kwamba Syria inalinda haki yake ya kuchukua fidia kutoka kwa Marekani kutokana na uporaji huo.

Ikumbukwe kuwa, katika wiki za hivi karibuni, Marekani imezidisha wizi wa mafuta ya Syria kwa ushirikiano na wanamgambo wa kundi la "Syrian Democratic Forces" (SDF) na kuhamishia mamia ya malori ya mafuta katika vituo vyake nchini Iraq.

Tags