Nabil Qaouk: Saudia hawauwezi muqawama wa Lebanon
Naibu wa Mkuu wa Baraza la Utendaji la Hizbullah ya Lebanon amesema kuwa, Saudi Arabia haiwezi kuushinda nguvu muqawama wa Lebanon.
Shirika la habari la IRNA limemnukuu Sheikh Nabil Qaouk akisema hayo katika sherehe maalumu zilizofanyika jana (Jumatatu) kusini mwa Lebanon na kusisitiza kuwa: Huenda Saudia ikafanikiwa kununua kwa fedha maamuzi ya jamii za kimataifa na nchi kubwa duniani, lakini haina uwezo kamwe wa kukabiliana na muqawama wa Lebanon.
Ameongeza kuwa, hatua ya Umoja wa Mataifa ya kuliondoa jina la Saudi Arabia katika orodha nyeusi ya nchi zinazokandamiza watoto, haiwezi kufuta aibu na jinai za ukoo wa Aal Saud katika fikra za walimwengu.
Sheikh Qaouk amesema, hadi hivi sasa Saudi Arabia inaendelea kufanya jinai nchini Yemen, na hilo walimwengu wanaliona wazi, hivyo hatua ya Umoja wa Mataifa ya kuliondoa jina la Saudia katika orodha ya madola yanayofanya jinai dhidi ya watoto nchini Yemen, haiwezi kuficha uhakika huo.
Aidha Naibu wa Mkuu wa Baraza la Utendaji la Hizbullah amesema, hatari za magenge ya kitakfiri imepungua nchini Lebanon kwa juhudi za jeshi na muqawama wa wananchi wa nchi hiyo, ingawa hata hivyo hatari hiyo bado ipo.