Nasrullah: Uvamizi wa kijeshi wa Israel dhidi ya Lebanon utajibiwa haraka
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i95430-nasrullah_uvamizi_wa_kijeshi_wa_israel_dhidi_ya_lebanon_utajibiwa_haraka
Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon amepuuzilia mbali vitisho vilivyotolewa hivi karibuni na maafisa wa utawala haramu wa Israel vya kuwepo uwezekano wa kuivamia kijeshi Lebanon na kusisitiza kuwa, uchokozi wowote wa Israel dhidi ya nchi hiyo ya Kiarabu utapata jibu la haraka.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 23, 2023 07:33 UTC
  • Nasrullah: Uvamizi wa kijeshi wa Israel dhidi ya Lebanon utajibiwa haraka

Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon amepuuzilia mbali vitisho vilivyotolewa hivi karibuni na maafisa wa utawala haramu wa Israel vya kuwepo uwezekano wa kuivamia kijeshi Lebanon na kusisitiza kuwa, uchokozi wowote wa Israel dhidi ya nchi hiyo ya Kiarabu utapata jibu la haraka.

Sayyid Hassan Nasrullah alisema hayo jana Jumatano katika hotuba yake aliyoitoa kwa njia ya televisheni baada ya Tel Aviv kuilamu Hizbullah kwa shambulio la bomu la siku chache zilizopita huko kaskazini mwa Israel.

Sayyid Nasrullah ameeleza bayana kuwa, iwapo vita vitatokea nchini Lebanon, hakuna shaka vitasambaa na kuenea katika zima la Asia Magharibi (Mashariki ya Kati).

Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amesema shambulio la Machi 13 huko kaskazini mwa mji wa Megiddo lilionyesha wazi kuwa utawala wa Kizayuni hivi sasa upo katika hali ya kudhoofika.

Amesema: Si jukumu letu kutoa majibu kwa mambo yanayomchanganya adui. Baadhi ya nyakati, kimya chetu ni sehemu ya vita vya kisakolojia mkabala wa maadui. Maafisa wa Israel wanaweza kwenda baharini wakitaka, lakini watambue kuwa sisi hatuogopi chochote. 

Wanajihadi wa Hizbullah ya Lebanon

Oktoba mwaka jana baada ya Sayyid Nasrullah kuonya kuwa iwapo Lebanon itanyimwa haki yake ya kufaidika na mafuta na gesi yake, basi hakuna yeyote atakayeweza kuchimba gesi katika medani ya Karish, utawala wa Kizayuni ulilazimika kukubali kutia saini makubaliano ya mpango wa kuchorwa mipaka ya baharini baina yake na Lebanon, hatua iliyoashiria ushindi mkubwa kwa Walebanon.

Sayyid Nasrullah alisema utawala huo ulisalimu amri kwani hauna uwezo wa kuingia vitani na Lebanon na hasa Hizbullah na kuonya kuwa, iwapo vita vitatokea basi yatakuwa ni majuto makubwa kwa utawala wa Kizayuni wa Israel.