Wananchi wa Uingereza wataka kufukuzwa balozi wa Israel mjini London
https://parstoday.ir/sw/news/world-i106988-wananchi_wa_uingereza_wataka_kufukuzwa_balozi_wa_israel_mjini_london
Wananchi wa Uingereza wametia saini waraka, wakitaka kufukuzwa balozi wa utawala wa Kizayuni wa Israel mjini London kwa sababu ya kuunga mkono mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Jan 09, 2024 04:18 UTC
  • Tzipi Hotovely
    Tzipi Hotovely

Wananchi wa Uingereza wametia saini waraka, wakitaka kufukuzwa balozi wa utawala wa Kizayuni wa Israel mjini London kwa sababu ya kuunga mkono mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza.

Kampeni hiyo ambayo imeyoandaliwa na Jukwaa la Dunia la Mabadiliko (The World’s Platform for Change) na kutiwa saini na zaidi ya watu laki moja, inatoa wito wa kufukuzwa balozi wa Israel nchini Uingereza, Tzipi Hotovely, kwa kuunga mkono mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza.

Waraka huo unasisitiza kuwa: Wakati jinai za utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan zikiendelea, balozi wa utawala huo ghasibu mjini London anaunga mkono waziwazi utekelezaji wa mauaji ya kimbari dhidi ya raia wa Palestina.

Inasemekana kwamba, kwa mujibu wa sheria za Uingereza, wakati raia wanaotetea jambo fulani nchini humo wanapopindukia watu laki moja, matakwa yao yanapaswa kujadiliwa na kuchunguzwa na wawakilishi wa Bunge.

Matamshi ya balozi wa utawala wa Kizayuni wa Israel mjini London na wito wake wa kufanyika mauaji ya kimbari dhidi ya wakazi wa Gaza, yameibua shutuma kwenye mitandao ya kijamii na kutambuliwa kama "wito wa wazi wa mauaji ya halaiki".

Israel inaendeleza mauaji ya kimbari Ukanda wa Gaza

Chris Doyle, Mkurugenzi wa Baraza la Maelewano la Waarabu na Uingereza, ameandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X kwamba: "Hii si kauli ya kwanza "ya uchochezi" ya balozi wa Israel mjini London, kwa sababu mwezi uliopita aliiambia televisheni ya Sky News kwamba: "Israel haitakubali kuanzishwa taifa huru la Palestina wala kusitisha vita katika Ukanda wa Gaza."

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, David Cameron alisema akijibu matamshi ya balozi wa Israel mjini London ambaye anapinga vikali suluhisho la kuanzishwa taifa huru la Palestina kwamba: Kauli hizi zinakatisha tamaa.