Jan 12, 2024 02:41 UTC
  • Kuanza kusikilizwa mashtaka ya Afrika Kusini katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki dhidi ya utawala wa Kizayuni

Mahakama ya Kimataifa ya Haki yenye makao makuu yake mjini The Hague Uholanzi Alhamisi na Ijumaa inasikiliza na kukusanya mitazamo ya kisheria ya Afrika Kusini na utawala wa Kizayuni kuhusu kesi ya mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza. Moja ya shughuli za mahakama hiyo ni kushughulikia mashtaka yanayohusiana na Mkataba wa Mauaji ya Kimbari wa 1948. Mkataba huo unatambuliwa rasmi na nchi 153.

Wizara ya Sheria ya Afrika Kusini ilitangaza katika taarifa yake kwamba kikao cha kwanza cha kusikilizwa mashataka ya nchi hiyo dhidi ya Israel kitafanyika Januari 11 na 12. Kwa mujibu wa  taarifa hiyo, Ronald Lamola, Waziri wa Sheria wa Afrika Kusini, anaongoza ujumbe wa wanasheria wa nchi hiyo huko The Haque. Mbali na kesi ya mauaji ya kimbari, Afrika Kusini pia imewasilisha ombi kwa Mahakama ya Kimataifa ya Haki kuzingatia hatua za muda au za kuzuia kukaririwa jinai hiyo. Nchi hiyo imeitaka mahakama hiyo itoe amri ya kuilazimisha  Israel isimamishe harakati hatua zake zote za kijeshi huko Gaza. Hii ni kesi ya dharura ambayo mahakama itaishughulikia kwanza.

Makao makuu ya Mahakama ya Haki mjini The Hague

Ikiwa moja ya nchi wanachama wa Mkataba wa Kuzuia na Kuadhibu jinai za Mauaji ya Kimbari, Afrika Kusini imejiwajibisha kuzuia kutokea kwa mauaji ya kimbari. Kwa hiyo, katika kikao maalum kilichofanyika  tarehe 8 Desemba, 2023, Baraza la Mawaziri la Afrika Kusini liliitaka Mahakama ya Kimataifa ya Haki iamuru Israel, ambayo pia ni mwanachama wake ijizuie  kuchukua hatua yoyote ya kijinai na ambayo ni kinyume na makubaliano ya mahakama hiyo. Kuhusiana na suala hilo, mnamo Desemba 29, 2023, ombi liliwasilishwa kwa Mahakama ya Kimataifa ya Haki, ambapo mahakama hiyo ilitakiwa kutangaza haraka kwamba kulingana na Mkataba wa Kuzuia Mauaji ya Kimbari, Israeli inakiuka majukumu yake na lazima isimamishe mara moja jinai na kuheshimu makubaliano hayo ya kimataifa. Mahakama ya Kimataifa ya Haki iliafikiana na malalamiko ya Afrika Kusini kuhusu ukiukaji wa Israel makubaliano ya mkataba huo. Ni kwa msingi huo ndipo Afrika Kusini, ikafungua kesi dhidi ya Israel kwa kuzingatia Mkataba wa Kuzuia Mauaji ya Kimbari. Elon Levy, Msemaji wa Baraza la Mawaziri la utawala haramu wa Israel alisema utajitetea vilivyo katika kesi hiyo. Wakati huo huo Marekani ambayo ni mshirika wa kimkakati wa Israel inaiunga mkono Tel Aviv kuhusiana na kesi ya Afrika Kusini ambapo John Kirby msemaji wa baraza la usalama wa taifa katika Ikulu ya White house ameitaja kesi hiyo kuwa "isiyo na thamani wala ushahidi wowote."

Afrika Kusini imeutaja utawala wa Kizayuni kuwa mtenda jinai na mauaji ya halaiki huko Gaza. Katika faili lenye kurasa 84 la Afrika Kusini, imeelezwa kuwa vitendo vya Israel vina utambulisho wa mauaji ya halaiki kwa sababu vinatekelezwa kwa lengo la kutokomeza kizazi cha Wapalestina huko Gaza. Faili la kesi hiyo limebainisha wazi kwamba vitendo vya mauaji ya halaiki ni pamoja na mauaji ya Wapalestina, kusababisha madhara makubwa ya kiakili na kimwili na kuandaliwa kwa makusudi mazingira yenye lengo la kuangamiza kimwili  kundi moja au kabila. Afrika Kusini imesisitiza kuwa kauli na matamshi ya viongozi wa Israel yanaonyesha kuwepo nia ya kutekeleza mauaji ya halaiki katika ukanda huo.

Juliet McIntyre, mhadhiri wa sheria katika Chuo Kikuu cha Australia Kusini, amesema kesi ya Afrika Kusini ni jumuishi kabisa na imeandaliwa kwa uangalifu mkubwa. Ameendelea kusema, kesi hiyo imeandaliwa kwa namna ambayo itajibu  pingamizi zozote zinazoweza kutolewa na Israeli na imezingatia madai yoyote ambayo yanaweza kutolewa kuhusu mahakama hiyo kutokuwa na mamlaka ya kuishughulikia kesi hiyo. Kabla ya kufungua kesi hiyo Pretoria ilikuwa imejadiliana suala hilo na Tel Aviv kwa njia mbalimbali ambapo ilikabiliwa na majibu hasi ya utawala wa Kizayuni katika uwanja huo.

Kufuatia hatua hiyo ya Afrika Kusini, Wizara ya Mambo ya Nje ya Israel katika taarifa yake Disemba 29 ilitoa radimali kuhusiana na jambo hilo. Tel Aviv pamoja na kuyapinga mashtaka hayo ilichukulia kufikishwa faili la Afrika Kusini dhidi yake katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki kuwa ni kashfa isiyo na msingi wala thamani yoyote ya kisheria na kudai kuwa inafuata sheria za kimataifa katika vita vyake dhidi ya Hamas huko Gaza.

Mauji ya halaiki ya Wazayuni dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza

Nukta muhimu ni kwamba baadhi ya nchi zimeonyesha nia ya  kujiunga na mashtaka hayo kufuatia malalamiko ya Afrika Kusini dhidi ya utawala wa Kizayuni katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki. Petra de Sutter, Naibu Waziri Mkuu wa Ubelgiji, alisema kwamba atapendekeza nchi yake ijiunge na malalamiko ya Afrika Kusini dhidi ya mauaji ya kimbari ya Israel huko Gaza. Ziyad Daghim, Balozi wa Libya nchini Uholanzi pia ametangaza kujiunga  nchi yake na kesi ya Afrika Kusini dhidi ya utawala wa Kizayuni na kusema: "Ubalozi huo utaendelea kushauriana na kutoa uuungaji mkono unaohitajika kwa timu ya wanasheria ya Afrika Kusini nchini Uholanzi.

Mashtaka ya Afrika Kusini dhidi ya Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki yameanda uwanja kwa nchi nyingine kuushtaki utawala huo katika mahakama za kimataifa ikiwemo Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC kwa kuzingatia jinai kubwa na zisizo na mfano wake zinazofanywa na Israel dhidi ya Wapalestina wasio na hatia katika Ukanda wa Gaza. Hasa ikizingatia kuwa Wapalestina elfu 23 wameuawa shahidi na wengine takriban elfu 60 wamejeruhiwa, wengi wao wakiwa wanawake na watoto kufuatia mashambulizi ya kinyama ya wanajeshi wa Kizayuni katika ukanda huo.

Tags