Mar 03, 2024 07:39 UTC
  • EU yaikosoa Israel kwa kuzuia misaada ya kibinadamu Gaza

Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya amekosoa hatua ya utawala haramu wa Israel ya kuzuia kuingizwa na kusambazwa misaada ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza.

Josep Borrell amesema hayo katika taarifa na kuongeza kuwa, mashambulizi yanayofanywa na Israel dhidi ya raia katika Ukanda wa Gaza hayahalalishika kwa namna yoyote ile.

Ameitaka Israel iheshimu sheria za kimataifa na iondoe vizuizi katika usambazaji wa misaada ya kibinadamu kwa raia wa eneo hilo lililo chini ya mzingiro.

Alkhamisi iliyopita, wanajeshi wa Israel waliwaua shahidi watu wasiopungua 115 waliokuwa katika umati uliokuwa ukisubiri kupatiwa misaada ya kibinadamu huko kusini mwa Gaza.

Mkuu wa Sera za Kigeni wa EU amegusia mauaji hayo na kueleza kuwa, mashambulizi ya Israel na kupuuzwa sheria za kimataifa kutapelekea kushadidi hali ya mambo na kuzuia kikamilifu usambazaji wa misaada ya kibinadamu.

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Ulaya ameongeza kuwa, Israel inapaswa kushirikiana na taasisi za Umoja wa Mataifa na mashirika yanayohusika na usambazaji wa misaada ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza.

Mgogoro wa kibinadamu Gaza

Kabla ya hapo, shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International lilitoa wito wa kufanyika uchunguzi wa haraka kuhusu mauaji hayo makubwa ya Wapalestina yaliyofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya raia wa Gaza waliokuwa wakisubiria kupokea misaada ya kibinadamu huko Gaza.

Aidha siku ya Ijumaa, Umoja wa Afrika ulilaani mauaji hayo huku ukitahadharisha kuhusu kutokea baa la njaa katika ukanda huo. Mwenyekiti wa Kamisheni ya AU,  Moussa Faki Mahamat amesema sababu kuu ya hali mbaya ya sasa ya Gaza ni mashambulizi ya kinyama ya Israel dhidi ya eneo hilo.

Tags