Mar 27, 2024 02:08 UTC
  • Soda ya 'Palestine Cola' yazinduliwa, mashirika ya Magharibi yaendelea kususiwa

Ndugu wawili wa Kipalestina wamezindua soda waliyoipa jina la 'Palestine Cola' na kusema kuwa, faida zote zitakazotokana na mauzo ya kinywaji hicho zitawaendea Wapalestina.

Mohamed Kiswani, Afisa Habari wa kampuni ya Safad Food AB inayozalisha kinywa hicho ameliambia shirika la habari la Anadolu kuwa, "Tumezindua bidhaa mbadala kwa yoyote anayeitaka...tumeanzisha kampuni inayowaunga mkono Wapalestina."

Kampuni hiyo yenye makao yake katika mji wa pwani wa Malmo, kusini mwa Sweden imesema soda ya Palestine Cola inaashiria nembo ya 'umoja na dhamira'.

Ndugu wawili wa Kipalestina Mohamed na Ahmad Hassoun waliyoanzisha kampuni ya Safad Food AB na kampuni dada ya 'Palestine Drinks' iliyozinduliwa mwezi uliopita wa Februari walifurushwa kwenye makazi yao katika mji wa Safad ulioko katika Wilaya ya Kaskazini katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu, wakati wa ukoloni wa Uingereza mwaka 1948.

Ndugu hao wa Kipalestina walilazimika kuishi kambini kama wakimbizi kusini mwa Lebanon, kabla ya kuhamia Sweden, ambapo baadaye walianzisha kampuni ya Safad Food AB.

Kususiwa bidhaa na kampuni zinazounga mkono jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel kumeandaa fursa kwa mashirika ya nchi za Kiislamu kuweza kuarifisha na kuuza bidhaa zao na hivyo kuimarisha uchumi wa nchi hizo.

Makampuni ya Magharibi kama vile McDonald's, Coca-Cola, Starbucks na KFC, ambayo yametangaza kuunga mkono utawala wa Kizayuni, yanakabiliwa na vikwazo kutoka kwa wananchi wa nchi kama vile Misri, Jordan, Oman, Kuwait, Qatar, UAE na Uturuki.

Kuimarikai kampeni ya kususiwa bidhaa na nembo mashuhuri za Israel, kumepelekea kuorodheshwa makumi ya makampuni na bidhaa za Magharibi zinazoisaidia Israel kwenye mitandao ya kijamii, na watu kutakiwa kununua bidhaa mbadala.

 

Tags