Mar 29, 2024 02:38 UTC
  • Kupokewa vizuri ripoti ya UN kuhusu mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israel huko Ghaza

Tathmini ya ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya Palestina juu ya mauaji ya umati yanayofanywa na Israel kwenye Ukanda wa Ghaza imepokewa vizuri na kuungwa mkono na wawakilishi wa nchi za dunia ndani ya umoja huo.

Katika ripoti na tathmini yake ya karibuni kabisa, Francesca Albanese, ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Palestina amesema kuwa jinai zinaendelea kufanywa na Israel tangu tarehe 7 Oktoba 2023 dhidi ya wakazi wa Ghaza zinaweza kuwaburuza viongozi wa Israel mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC na kuwashughulisha na kesi nyingi dhidi yao kwa miaka 50 ijayo kutokana na mfumo wa hivi sasa wa mahakama hiyo.

Albanese amewasilisha ripoti yake hiyo ya karibuni kabisa mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kusisitiza kuwa, hivi sasa utawala wa Kizayuni unafanya mauaji ya kimbari kwenye Ukanda wa Ghaza. Baada ya kusomwa ripoti ya ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Ghaza mbele ya Baraza la Usalama, wajumbe wa baraza hilo wakiwemo wawakilishi kutoka nchi za Misri, Pakistan, Qatar, Russia, Iran na China wameunga mkono ripoti hiyo. Kwa upande wake Umoja wa Ulaya umetaka kufanyike uchunguzi huru na unaofaa kuhusu shutuma zote dhidi ya Israel zilizomo kwenye ripoti hiyo. Umoja huo umedai kuwa umeshtushwa na kiwango kikubwa cha maafa ya kibinadamu kinachoshuhudiwa kwenye Ukanda wa Ghaza hivi sasa. 

Jamii ya kimataifa yalaani jinai za Israel dhidi ya Wapalestina

 

Tangu tarehe 7 Okbota 2023, utawala wa Kizayuni wa Israel umekuwa ukifanya mauaji ya kutisha dhidi ya Wapalestina wa Ghaza kwa uungaji mkono kamili wa baadhi ya Madola ya Magharibi hasa Marekani, Uingereza na Ujerumani. Jinai hizo wanafanyiwa pia Wapalestina wanaoishi kwenye Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan. Hadi tunaandika uchambuizi huu wa kisiasa, zaidi ya Wapalestina 32,000 walikuwa wameshauawa shahidi na zaidi ya 74,000 wengine walikuwa wameshajeruhiwa kutokana na jinai hizo za kutisha za Israel. Jinai hizo zimepelekea utawala wa Kizayuni uburuzwe kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC kwa shutuma za kufanya mauaji ya wazi kabisa ya kizazi.

Nayo Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC ilitoa hukumu tarehe 29 Septemba 2023 ya kesi iliyofunguliwa na Afrika Kusini dhidi ya Israel na kuuamrisha utawala wa Kizayuni uache kufanya mauaji ya kimbari na kushambulia raia huko Ghaza. Mahakama hiyo iliiamrisha Israel ikabidhi ripoti yake kuhusu utekelezaji wa amri ya mahakama hiyo katika kipindi cha mwezi mmoja tangu ilipotolewa. Lakini kutokana na utawala wa Kizayuni kuungwa mkono kikakmilifu na Marekani, hadi hivi sasa umedharau amri hiyo ya mahakama ya ICC na si tu haujasita kufanya mauaji ya raia wasio na hatia lakini pia umekuwa ukiushambulia mji wa Rafah ambao una idadi kubwa ya raia waliokimbilia mji huo hasa kutoka kaskazini mwa Ghaza ambako Israel imefanya mashamblizi ya kinyama na kikaktili mno dhidi ya Wapalestina. Si hayo tu lakini pia utawala wa Kizayuni umefunga njia zote za kuingia na kutoka kwenye Ukanda wa Ghaza na umepiga marufuku kuingia misaada ya kibinadamu na huduma nyingine zote za dharura na za lazima za kumuwezesha mtu kuishi.

Subira ya kihistoria ya Wapalestina imewafedhehesha Wazayuni

 

Lakini wananchi wa Palestina hawajatetereka katika imani yao licha ya kukumbwa na jinai kubwa zaidi katika historia na mauaji makubwa zaidi ya umati yanayoungwa mkono na Marekani huko Ghaza. Matukio ya hivi  karibuni ya Ukanda wa Ghaza yameufedhehesha utawala wa Kizayuni, Marekani na baadhi ya nchi za Magharibi ambazo huko nyuma zilikuwa zinajifanya kuwa zinapigania haki za binadamu na eti ni tawala za kiungwana. Kwa subira ya kihistoria ya wananchi wa Ghaza, dunia nzima hivi sasa imeelewa kuwa madai ya madola ya Magharibi ya kupigania haki za binadamu na kuheshimu damu za raia ni uongo mtupu, na huu unahesabiwa kuwa ni miongoni mwa ushindi mkubwa waliopata Wapalestina kupitia operesheni yao ya kihistoria ya Kimbunga cha al Aqsa.

Tags