Mar 29, 2024 02:38 UTC
  • Erdogan: Dunia iishinikize Israel itekeleze azimio la Baraza la Usalama la UN

Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan ameitaka jamii ya kimataifa iendelee kuushinikiza utawala wa Kizayuni wa Israel utekeleze azimio la kutaka kusitishwa mara moja mapigano huko Gaza, lililopasishwa majuzi na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Erdogan alitoa mwito huo jana Alkhamisi akihutubia mkutano wa kampeni za uchaguzi katika mkoa wa Batman, mashariki mwa Uturuki na kuongeza kuwa: Lazima mashinikizo yaongezwe dhidi ya Israel, mwanaharamu na mwana mdekezwa wa Magharibi ili iheshimu azimio hilo.

Jumatatu iliyopita, wanachama 14 kati ya 15 wa Baraza la Usalama la UN walilipigia kura ya ndio azimilo lililowasilishwa na nchi wanachama wa kudumu wa baraza hilo kwa ajili ya kusitisha vita haraka katika Ukanda wa Gaza. Marekani ambayo ni mwanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama haikupiga kura ya turufu tofauti na huko nyuma, na kwa utaratibu huo azimio la kusitisha vita Gaza likawa limepasishwa. 

Rais wa Uturuki amesema taifa lake litafanya jitihada za kuhakikisha kuwa utawala wa Israel unafungamana na azimio hilo la kusitisha vita katika mwezi huu wa Ramadhani, huku akiyataka mataifa mengine ya dunia yatekeleze wajibu wao wa kuiwekea mashinikizo Tel Aviv.

Kikao cha Baraza la Usalama la UN

Erdogan ameeleza bayana kuwa, Uturuki itaendelea kufanya juhudi kuhakikisha kuwa dunia inaitambua Israel kama dola la kigaidi na kuongeza kuwa, Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS si kundi la magaidi, bali ni kundi la wapigania ukombozi.

Kadhalika ametoa mwito kwa mataifa ya Waislamu kushirikiana na kuwa kitu kimoja katika kukomesha jinai za kutisha zinazoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina wa Gaza.

Tags