May 23, 2024 07:20 UTC
  • Marekani kuipa Kenya hadhi ya mshirika wake mkuu asiye mwanachama wa NATO

Rais Joe Biden wa Marekani anatarajiwa kuipa Kenya hadhi ya mshirika wake mkuu asiye mwanachama wa NATO wakati wa ziara ya kiserikali ya siku tatu ya Rais wa Kenya William Ruto nchini humo, ambaye amekaribishwa na Biden katika Ikulu ya White House mapema leo kabla ya mapokezi rasmi yatakayoanza kwa ukaguzi wa gwaride la heshima na kufikia kielele chake kwa dhifa ya kifahari ya chakula cha usiku.

Kenya itakuwa nchi ya kwanza ya Afrika, kusini mwa Jangwa la Sahara kupatiwa hadhi hiyo, ikionyesha msukumo wa Washington wa kuimarisha uhusiano na taifa hilo la Afrika Mashariki, ambalo limekuwa na uhusiano wa karibu pia na Russia na China likijiandaa kutuma askari wake 1,000 nchini Haiti kama sehemu ya kikosi cha Umoja wa Mataifa kushughulikia mzozo wa usalama katika nchi hiyo ya eneo la Carribean.
 
Nchi nyingine zinazotarajiwa kuvisaidia vikosi vya Kenya katika operesheni hiyo ni pamoja na Bahamas, Barbados, Benin, Chad na Bangladesh.
 
Hadhi ya kuwa mshirika mkuu wa Marekani asiye mwanachama wa NATO hupatiwa nchi yenye ukuruba na Washington na yenye uhusiano wa kimkakati wa kiutendaji na jeshi la nchi hiyo.
Biden (kulia) na Ruto katika mkutano na viongozi wa wafanyabiashara wa Marekani na Kenya

Mnamo mwezi Machi, Biden aliipatia Qatar hadhi hiyo ya mshirika mkuu wa Marekani asiye mwanachama wa NATO akitimiza ahadi ambayo alikuwa ameitoa kwa nchi hiyo mwanzoni mwa mwaka.

 
Uamuzi huo wa Biden umetangulia kutangazwa na maafisa wawili wa Marekani ambao hawakutaka kutajwa majina yao likiwa ni dokezo la tangazo litakalokuja kutolewa baadaye wakati wa ziara ya Ruto, ambayo ilianza kwa mkutano uliofanyika katika Ikulu ya White House jana Jumatano jioni na viongozi wa wafanyabiashara wa Marekani na Kenya.../

 

Tags