UN yakosoa azma ya Israel ya kujenga sinagogi katika Msikiti wa al-Aqsa
(last modified Tue, 27 Aug 2024 12:18:34 GMT )
Aug 27, 2024 12:18 UTC
  • Stephane Dujarric
    Stephane Dujarric

Msemaji wa Umoja wa Mataifa amekosoa vikali pendekezo lililotolewa hivi karibuni na Waziri wa Usalama wa Israel, Itamar Ben Gvir, la kutaka kujenga sinagogi ndani ya Msikiti wa Al-Aqsa.

Stephane Dujarric amesema katika kikao na waandishi wa habari kuwa, "kauli za aina hii hazina tija wala maana. Zinazidisha hatari ya kushadidisha hali ambayo tayari ni mbaya."

Huku akishiria unyeti unaoyazunguka maeneo matakatifu katika mji wa Quds (Jerusalem), Dujarric amesema, kuna mwafaka uliokubaliwa na pande zote wa kutaka kuheshimiwa maeneo matakatifu ya Quds na wahusika wote.

Juzi Jumatatu, Waziri wa Usalama wa Israel, Itamar Ben Gvir alitangaza katika mahojiano yake na kituo cha redio cha jeshi la Israel (Galei Zahal), nia yake ya kuanzisha sinagogi katika Msikiti wa Al-Aqsa, licha ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu kusisitiza kwamba, hakuna mabadiliko katika hali ya sasa ya Msikiti wa Al-Aqsa. 

Wazayuni wakiivunjia heshima Aqswa

Waziri wa Usalama wa Ndani wa Israel aliiambia redio hiyo kwamba, "kama nitaweza kufanya kile ninachonuia, nitajenga sinagogi kwenye Mlima wa Hekalu." 

Stephane Dujarric, Msemaji wa Umoja wa Mataifa anasisitiza kuwa, kuna haja ya kuheshimiwa makubaliano ya kuheshimu maeneo matukufu mjini Quds, na kujiepusha na vitendo na matamshi yanayoweza kuchochea moto wa taharuki katika eneo la Magharibi mwa Asia.

Tags