UN yataka kutumwa askari wa kulinda amani Sudan Kusini
(last modified Wed, 14 Dec 2016 14:14:38 GMT )
Dec 14, 2016 14:14 UTC
  • UN yataka kutumwa askari wa kulinda amani Sudan Kusini

Umoja wa Mataifa umetoa wito wa kutumwa askari wa kulinda amani nchini Sudan Kusini, ili kuzuia nchi hiyo isitumbukie katika mauaji ya kimbari kama yale yaliyoshuhudiwa nchini Rwanda mwaka 1994.

Wito huo umetolewa hii leo na Yasmin Sooka, Mjumbe wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, katika kikao cha dharura cha baraza hilo mjini Geneva na kufafanua kuwa, iwapo jamii ya kimatifa inataka Sudan Kusini isitumbukie katika mauaji ya kimbari, basi sharti askari 4,000 wa kulinda amani watumwe nchini humo haraka iwezekanavyo.

Aidha ametoa wito wa kuundwa mahamaka maalumu ya kuwashtaki watenda jinai katika nchi hiyo changa zaidi barani Afrika na kubainisha kuwa, iwapo hatua hizo za dharura hazitachukuliwa, yumkini mgogoro unaoshuhudiwa nchini Sudan Kusini ukawa na taathira hasi kwa eneo lote.

Zeid Ra'ad al Hussein, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa

Kwa upande wake, Zeid Ra'ad al Hussein, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amelitaka Baraza la Haki za Binadamu la umoja huo kuhakikisha kuwa, mahakama hiyo maalumu inabuniwa ili kuwawajibisha wahusika wa jinai za kivita nchini Sudan Kusini.

Siku chache zilizopita, Yasmin Sooka, Mjumbe wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini alisema maeneo kadhaa ya nchi hiyo yameshuhudia matukio ya uangamizaji wa kikabila. 

Mauaji ya kutisha nchini Sudan Kusini

Sooka aliyasema hayo baada ya safari yake ya siku 10 aliyofanya nchini Sudan Kusini na kubainisha kuwa, mazingira yaliyopo nchini humo hivi sasa yanafanana na yale yaliyokuwepo nchini Rwanda kabla ya mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 na kusisitiza kuwa, kuna uwezekano hali hiyo ikageuka na kuwa mauaji ya kimbari.