Aug 15, 2017 07:13 UTC
  • Russia: Kampeni ya US huko Afghanistan imefeli, iondoe askari wake

Mjumbe maalumu wa Rais wa Russia nchini Afghanistan amesema kampeni na uwepo wa vikosi vya Marekani nchini Afghanistan haujawa na tija yeyote hadi sasa na kwa msingi huo Washington inafaa kuwaondoa wanajeshi wake nchini humo mara moja.

Zamir Kabulov ameliambia gazeti la Izvestia kuwa, uwepo wa Marekani nchini Afghanistan umefeli na Moscow haioni haja wala udharura wa askari wa US kuendelea kubakia nchini humo.

Kabulov ambaye pia ni Mkurugenzi wa masuala ya Asia katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia amesema: "Kampeni ya Marekani nchini Afghanistan imegonga mwamba, bora iondoe vikosi vyake kikamilifu. Afghanistan ipo katika hatari ya kuwa mzalishaji na mlezi mkubwa wa ugaidi wa kimataifa."

Haya yanajiri katika hali ambayo, karibuni hivi Rais Donald Trump wa Marekani alisema nchi yake ipo katika hatua za mwisho za kutangaza stratejia mpya eti ya 'kupambana na ugaidi' nchini Afghanistan.

US pia inatuhumiwa kuwa chanzo cha uzalishaji wa mihadarati Afghanistan

Siku tatu zilizopita, raia 16 waliuawa katika shambulizi la anga la muungano wa kijeshi wa nchi za Magharibi unaoongozwa na Marekani nchini Afghanistan, ikiwa ni muendelezo wa hujuma za anga za muungano huo unaodai kupambana na magenge ya kigaidi.

Marekani yenye wanajeshi 8,400 nchini Afghanistan imekuwa ikiihadaa jamii ya kimataifa kuwa inapambana na ugaidi katika nchi hiyo ya Mashariki ya Kati, licha ya duru mbalimbali za habari kuarifu kuwa, Washington imekuwa ikiyapa silaha magege ya kigaidi nchini humo.

Tags