Korea Kaskazini yavurumisha makombora ya balistiki
https://parstoday.ir/sw/news/world-i33642-korea_kaskazini_yavurumisha_makombora_ya_balistiki
Korea Kaskazini imevurumisha makombora matatu ya masafa mafupi ya balistiki kuelekea pwani yake ya kaskazini.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Aug 26, 2017 07:01 UTC
  • Korea Kaskazini yavurumisha makombora ya balistiki

Korea Kaskazini imevurumisha makombora matatu ya masafa mafupi ya balistiki kuelekea pwani yake ya kaskazini.

Kamandi ya Pasikifi ya Jeshi la Marekani imethibitisha kuwa makombora hayo yaliyovurumishwa mapema leo Jumamosi hayakuwa tishio kwa Amerika Kaskazini na Kisiwa cha Guam kinachomilikiwa na Marekani.

Jeshi la Korea Kusini nalo limetoa taarifa na kusema Korea Kaskazini imevurumisha makombora kadhaa kutoka katika mkoa wa Kangwon na kwamba yaliruka umbali wa kilomita 250 kabla ya kutua baharini katika pwani ya mashariki mwa nchi hiyo. Marekani imedai kuwa makombora hayo matatu yamefeli katika majaribio.

Urushaji makombora hayo Jumamosi ni wa kwanza kutekelezwa na Korea Kaskazini tokea Julai 28 wakati ilipofanyia majaribio kombora ililososema linaweza kusafiri umbali wa kilomita 10,000 na kulenga baadhi ya maeneo ya Marekani.

Makombora ya Korea Kaskazini katika maonyesho ya kijesi

Siku ya Jumatano, kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un aliamuru uundwaji wa makombora zaidi baada ya Marekani kudai kuwa vitisho vyake vimefanikiwa kubadilisha mwenendo wa Pyongyang.

Katika wiki za hivi karibuni kumekuwa na wasi wasi wa kuanza vita baina ya Marekani na Korea Kaskazini kutokana na matamshi ya kivita ya viongozi wa nchi hizo mbili. Aidha Korea Kaskazini imekasirishwa na hatua ya Marekani kufanya mazoezi ya kijeshi na Korea Kusini katika Peninsula ya Korea.