US yaanzisha tena chokochoko katika Peninsula ya Korea
https://parstoday.ir/sw/news/world-i35511-us_yaanzisha_tena_chokochoko_katika_peninsula_ya_korea
Kwa mara nyingine tena Marekani imefanya maneva ya kijeshi kwa kushirikiana na Korea Kusini na Japan katika Peninsula Korea.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Oct 11, 2017 08:19 UTC
  • US yaanzisha tena chokochoko katika Peninsula ya Korea

Kwa mara nyingine tena Marekani imefanya maneva ya kijeshi kwa kushirikiana na Korea Kusini na Japan katika Peninsula Korea.

Jeshi la Marekani limerusha katika anga ya eneo hilo ndege zake za kivita aina ya supersonic B-1B, zenye uwezo mkubwa wa kudondosha mabomu. Aidha Korea Kusini imerusha ndege za mbili aina ya F-15K huku Japan ikirusha F-15.

Kikosi cha Anga cha Pacific cha Marekani (PACAF) kimesema ndege hizo zimeruka katika anga ya maji ya bahari ya Japan jana Jumanne. 

Hii sio mara ya kwanza kwa Marekani na Korea Kusini kufanya maneva ya pamoja ya kijeshi kaskazini mwa Korea Kusini.

Ndege za US katika anga ya Korea

Mwishoni mwa mwezi Agosti mwaka huu, Marekani na Korea Kusini zilifanya luteka ya siku 10 licha ya serikali ya Pyongyang kutoa onyo kali kwa nchi hiyo. Maneva hayo yaliwashirikisha askari elfu 17,500 wa Marekani na wengine elfu 50 wa Korea Kusini.

Hivi karibuni, gazeti la Rodong Sinmun la chama tawala nchini Korea Kaskazini liliandika kuwa, mkataba wa kijeshi wa hivi karibuni kati ya US na Seoul ni njama ya wazi ya Marekani na mshirika wake Korea Kusini kwa ajili ya kufanikisha ndoto zao za kutaka kuishambulia ardhi ya nchi hiyo.