Uislamu kuwa dini ya pili kwa ukubwa nchini Marekani 2040
Uchunguzi uliofanywa na kituo cha utafiti cha Pew nchini Marekani umeonesha kuwa, idadi ya Waislamu nchini humo itakuwa ya pili kwa ukubwa, baada ya Ukristo kufikia mwaka 2040.
Kwa mujibu wa ripoti ya kituo hicho, idadi ya Waislamu nchini humo inaongezeka kwa wastani wa watu laki moja kila mwaka.
Uchunguzi wa Pew umesema idadi ya Waislamu nchini Marekani itaongezeka na kuipiku ile ya Mayahudi.
Kwa mujibu wa kituo hicho, kufikia mwishoni mwa mwaka uliomalizika wa 2017, idadi ya Waislamu wanaoishi Marekani 'kihalali' ilikuwa milioni 3.4.
Hata hivyo takwimu za taasisi huru za Kiislamu nchini humo kama vile Baraza la Mahusiano ya Kiislamu Marekani (CAIR) zinaonyesha kuwa, kuna Waislamu kati ya milioni 6 na 8 nchini humo.
Mwaka uliopita, uchunguzi mwingine uliofanywa na kituo cha utafiti cha Pew nchini Marekani ulionesha kuwa, Uislamu utashika nafasi ya Ukristo kwa kuwa na idadi kubwa zaidi ya wafuasi duniani baada ya mwaka 2050.