May 18, 2018 14:00 UTC
  • Mkuu wa haki za binadamu wa UN ataka kuchunguzwa jinai za kivita za Israel

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa ametoa mwito wa kufanywa uchunguzi huru juu ya mauaji ya raia wa Kipalestina wa Ukanda wa Ghaza yaliyofanywa hivi karibuni na wanajeshi wa utawala wa Kizayuni.

Zeid Ra'ad al-Hussein ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa kikao maalumu cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa mjini Geneva leo Ijumaa na kufafanua kuwa, Israel imekiuka wazi na kwa mpangilio maalumu haki za Wapalestina, na haswa wakazi milioni 1.9 wa Ghaza, wanaoshi katika mzingiro; huku akisisitizia haja ya kufanywa uchunguzi juu ya jinai za kivita za Israel.

Kwa mujibu wa Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Wapalestina zaidi ya 100 wameuawa katika Ukanda wa Ghaza ndani ya wiki sita zilizopita, kwa kufyatuliwa risasi na wapiga shabaha wa Israel (Snippers), na kwamba hakuna ushahidi wenye mashiko unaoyapa nguvu madai ya Tel Aviv kwamba jeshi lake lilijitahidi kadri ya uwezo wake lisisababishe madhara makubwa kwa waandamanaji wa Kipalestina huko Ghaza.

Wapalestina wakibeba miili ya baadhi ya Mashahidi wa Gaza

Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa juzi lilitoa taarifa ya kulaaniukatili huo wa utawala haramu wa Israel, hatua ambayo ilimhamakisha Avigdor Lieberman, Waziri wa Vita wa utawala wa Kizayuni ambaye alisema Tel Aviv inapaswa kujiondoa kwenye baraza hilo haraka iwezekanavyo. 

Aidha Jumuiya ya Nchi za Kiarabu imetaka kufanyika uchunguzi wa kimataifa kuhusiana na jinai za hivi karibuni za utawala katili wa Israel dhidi ya Wapalestina katika eneo la Ukanda wa Ghaza.

Mbali na Wapalestina 64 kuuawa shahidi katika maandamano ya Jumatatu, wengine zaidi ya 2,700 walijeruhiwa katika mauaji hayo ya umati ambayo yalitekelezwa na askari wa utawala katili wa Israel, katika Ukanda wa Ghaza.

Tags