Kukaririwa tuhuma zisizo na msingi za Marekani dhidi ya Iran
Katika kipindi chote cha miaka 40 ya kuasisiwa mfumo wa Jamhuriya Kiislamu nchini Iran, Marekani daima imekuwa ikifuatilia na kutoa tuhuma maalumu na zisizo na msingi dhidi ya taifa la Iran.
Moja ya tuhuma hizo ni kuituhumu Iran kuwa inaunga mkono ugaidi na hivyo kuchukua hatua nyingi za kiuadui dhidi ya nchi hii. Baad ya Rais Donald Trump wa Marekani kuitoa nchi hiyo katika mapatano ya kimataifa ya nyuklia yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji, JCPOA mnamo tarehe 8 Mei mwaka huu, katika hatua iliyofuata, Mike Pompeo, Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo naye alitangaza masharti 12 yanayopaswa kutekelezwa na serikali ya Tehran kabla ya eti nchi hiyo kufanya mazungumzo na Iran. Masharti hayo ndio chanzo kikuu cha tofauti kati ya Marekani na nchi nyingine za kundi la 5+1. Hii ni kwa sababu mbali na kuwa msharti hayo yanadhihirisha matakwa ya kibabe ya Marekani kuhusiana na uwezo wa nishati ya nyuklia wa Iran, pia yanaweka wazi matakwa mapya na ya ziada ambayo yako nje ya mapatano ya JCPOA. Kuhusu hilo Marekani inataka kusimamishwa mpango mzima wa nyuklia wa Iran, miradi yake ya makombora na kusimamishwa siasa na hatua zote za Iran katika nchi za eneo kukiwemo kukatwa misaada ya Tehran kwa makundi yanayotuhumiwa kuwa ya kigaidi.
Ijumaa, Pompeo kwa mara nyingine tena alikariri tuhuma hizo zisizo na msingi dhidi ya Iran na kudai kuwa Iran inaunga mkono ugaidi na kuvuruga usalama wa eneo kwa kueneza silaha katika Mashariki ya Kati na maeneo mengine ya dunia. Huku akiunga mkono siasa za kiuadui za Trump dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Pompeo amedai kuwa siasa hizo zinatokona na maoni na ushauri wa timu ya kitaalamu ambayo imepewa jukumu la kufuatilia masuala ya Iran. Pompeo vilevile amewataka washirika wa Marekani kushirikiana na Trump katika kutekeleza siasa zake zinazolenga kutoa mashinikizo zaidi dhidi ya serikali ya Tehran. Tuhuma za uungaji mkono zinatolewa dhidi ya Iran katika hali ambayo Marekani yenyewe ndiyo muungaji mkono mkuu wa ugaidi katika Mashariki ya Kati na maeneo mengine ya dunia na hasa tukitilia maanani kwamba nchi hiyo ndiyo mwanzilishi na mdhamini mkuu wa makundi hatari ya kigaidi na hasa Daesh kwa ushirikiano wa marafiki zake wa kieneo wakiongozwa na Saudi Arabia. Hii ni katika hali ambayo Iran imekuwa mstari wa mbele wa kupambana na makundi hayo yanayoongozwa na Daesh katika eneo. Makundi hayo ambayo yanachukuliwa kuwa washirika wakuu wa Marekani na Saudi Arabia katika Mashariki ya Kati, yametekeleza jinai na mauaji ya kutisha kieneo na kimataifa kwa msaada wa moja kwa moja wa tawala za Washington na Riyadh.
Huu ni ukweli ambao Trump mwenyewe anakubaliana nao. Katika kampeni zake za uchaguzi Januari mwaka 2016, Trump alimkosoa Rais Barack Obama na Waziri wake wa Mambo ya Nje, Hillary Clinton kwa kuasisi kundi la kigaidi la Daesh kwa ushirikiano wa karibu wa Saudi Arabia. Ni kutokana na ushirikiano huo muovu ndipo nchi za Syria na Iraq zikashuhudia wimbi kubwa la matukio ya uharibifu wa nchi, ghasia mauaji ya kutisha na jinai ngingine nyingi kutokana na vitendo vya mabavu vya kundi hilo la kigaidi. Lengo la Marekani na washirika wake wa kieneo na Kimagharibi la kuunga mkono kundi hilo la kigaidi na kitakfiri ni kukabiliana moja kwa moja na mrengo wa mapambano ya Kiislamu katika eneo, ambapo Syria ni moja ya nguzo zake muhimu. Mwishoni mwa mwezi Disemba 2017 kundi moja la wataalamu wa kiintelijensia wa Marekani walimwandikia barua Trump wakimkosoa vikali kwa kuituhumu Iran kuwa inaunga mkono ugaidi na kusisitiza kuwa Saudia ndiyo muungaji mkono mkuu wa ugaidi katika eneo.
Iran ikiwa ni muhanga mkuu wa ugaidi, imekuwa mstari wa mbele katika kupambana na ugaidi na ili kukabiliana vilivyo na makundi hatari ya kigaidi yanayoungwa mkono moja kwa moja na Marekani na washirika wake katika nchi za Syria na Iraq, imekuwa ikitoa ushuri wa kijeshi kwa majeshi ya nchi hizo mbili za Kiarabu tena kwa idhini yao rasmi, kinyume na wanavyofanya wavamizi wa Kimarekani na washirika wao katika nchi hizo. Ushauri huo wa kijeshi wa Iran kwa nchi hizo bila shaka umewakasirisha sana watawala wa Marekani, Israel na Saudia. Licha ya hayo yote katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inachukulia uungaji mkono na msaada kwa mataifa yanayopigania uhuru na ukombozi wao kuwa moja ya majukumu yake muhimu, na ndio maana imekuwa ikiyaunga mkono waziwazi makundi kama vile Hizbullah ya Lebanon na Hamasa ya Palestina kwa ajili ya kupambana na uvamizi na uchokozi wa mara kwa mara wa utawala haramu wa Israel.