Uamuzi wa Trump wa kuondoka askari wa Marekani nchini Syria
https://parstoday.ir/sw/news/world-i50300-uamuzi_wa_trump_wa_kuondoka_askari_wa_marekani_nchini_syria
Baada ya kuanza mgogoro wa Syria mwaka 2011, Marekani kama kinara wa nchi za Magharibi ikishirikiana na Italia na Ufaransa katika jitihada za kutimiza malengo ya Magharibi na baadhi ya nchi za Kiarabu ya kutaka kuangamiza kambi ya mapambano Mashariki ya Kati na kuiondoa madarakani serikali halali ya Syria, ilijikita zaidi katika suala la kuyasaidia makundi ya kigaidi na waasi wanaobeba silaha kwa ajili ya eti kuiondoa madarakani serikali ya Rais Bashar Assad.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 20, 2018 07:06 UTC
  • Uamuzi wa Trump wa kuondoka askari wa Marekani nchini Syria

Baada ya kuanza mgogoro wa Syria mwaka 2011, Marekani kama kinara wa nchi za Magharibi ikishirikiana na Italia na Ufaransa katika jitihada za kutimiza malengo ya Magharibi na baadhi ya nchi za Kiarabu ya kutaka kuangamiza kambi ya mapambano Mashariki ya Kati na kuiondoa madarakani serikali halali ya Syria, ilijikita zaidi katika suala la kuyasaidia makundi ya kigaidi na waasi wanaobeba silaha kwa ajili ya eti kuiondoa madarakani serikali ya Rais Bashar Assad.

Hata hivyo tofauti na ndoto hizo, nchi hizo zimefeli na kushindwa kutimzia malengo yao baada ya vita vya karibu miaka 7. Kwa msingi huo tunaweza kusema kuwa, Washington imefeli na kushindwa kutekeleza njama zake nchini Syria hususan mpango wa kusimika serikali mbadala itakayokuwa mwanasesere na kibaraka wa nchi za Magharibi. 

Katika upande mwingine ni kuwa, tangu katikati ya mwaka 2014 na kwa kisingizio cha kupambana na makundi ya kigaidi, serikali ya Washington ilianzisha kilichopewa jina la muungano wa kimataifa wa kupambana na kundi la Daesh na mashambulizi yaliyofanywa na muungano huo yamekuwa yakiua idadi kubwa ya raia wasio na hatia nchini Syria. Baada ya hapo jeshi al Marekani lilipelekwa katika maeneo ya kaskazini na kaskazini mashariki mwa Syria na sasa Marekani ina karibu askari elfu mbili katika ardhi ya nchi hiyo. Idadi kubwa ya askari hao ni wa kikosi cha operesheni maalumu wanaoshirikiana na waasi wa Kikurdi na wale wa Kiarabu wanaojiita Syrian Democratic Forces.

Rais Donald Trump wa Marekani ambaye ni mashuhuri kwa kuchukua maamuzi ya kutatanisha na yasiyotabirika, Jumatano ya jana alijitokeza ghafla na kutangaza kwamba, ataliondoa jeshi la Marekani nchini Syria. Trump amedai katika ukurasa wake wa mtandao wa Twitter kwamba: "Tumelishinda kundi la Daesh nchini Syria na hiyo ndiyo iliyokuwa sababu pekee ya kuwepo jeshi la Marekani nchini humo katika kipindi cha uongozi wa Trump." Kiongozi huyo wa Marekani pia ameandika kuwa: "Baada ya ushindi wa kihistoria katika vita na Daesh, sasa umewadia wakati wa kuondoa jeshi letu nchini Syria na kulirejesha nyumbani."

Hata hivyo madai hayo ya Trump kuhusu kulishinda kundi la kigaidi la Daesh na uamuzi wake wa kuliondoa jeshi la Marekani nchini Syria vimepuuzwa katika duru za ndani na pia waitifaki wa Marekani. Si hayo tu bali seneta maarufu wa Marekani Lindsey Graham amekadhibisha madai ya Rais Donald Trump kwamba Marekani imelishinda kundi la kigaidi la Daesh na kusema hiyo ni habari bandia (fake news). Lindsey Graham ameitaja hatua ya kuliondoa jeshi la nchi hiyo huko Syria kuwa ni doa baya kwa Marekani.  

Lindsey Graham

Nader Entessar ambaye ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Alabama anasema: "Uamuzi huu wa Marekani au bora tuseme uamuzi wa Trump haukutarajiwa katika kipindi cha sasa na umezusha mshtuko katika siasa za nje za Marekani."

Uamuzi uliochukuliwa na Donald Trump wa kuliondoa ghafla jeshi la Marekani nchini Syria unaweza kutazamwa na kutathmini kwa mitazamo mbalimbali. Kwanza kabisa ni kwamba, Donald Trump kama ulivyo uamuzi wenyewe, ni mtu asiyetabirika na amechukua misimamo na maamuzi yasiyotabirika kama haya mara kadhaa katika kipindi hiki cha utawala wake. Miongoni mwa maamuzi hayo ni ule wa kukutana na kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong-un.

Ni vyema kusema hapa kuwa, Trump daima huwa hatekelezi maamuzi yake yasiyotarajiwa na ya kushtukiza na pale anapokabiliwa na upinzani mkali au kutambua kwamba utekelezaji wa maamuzi hayo utakuwa na gharama kubwa, hurudi nyuma na kuyatupilia mbali; mfano wake ni bajeti ya dola bilioni tano ya kujenga ukuta katika mpaka wa nchi hiyo na Mexico, suala ambalo ameamua kuliacha baada ya kukabiliwa na upinzani wa Kongresi.

Kuhusu uamuzi wake wa kuliondoa jeshi la Marekani nchini Syria inatupasa kusubiri na kuona je, Trump atabadili uamuzi huo baada ya kukabiliwa na upinzani mkali wa Pentagon, Kongresi na baadhi ya waitifaki wa Marekani kama utawala haramu wa Israel, au atautekeleza licha ya upinzani huo?

Donald Trump

Miongoni mwa mambo yanayoweza kuwa sababu za uamuzi wa Trump kuhusu Syria ni kwamba, wanastatijia wa Kimarakeni wanaamini kuwa, Washington haitaweza kubadilisha mlingano wa nguvu nchini Syria katika kipindi kifupi bila ya kulipa gharama kubwa na kwamba, ni bora kwa Marekani kuondoka nchini humo.

Yumkini sababu nyingine ikawa ni kwamba, kwa kutilia maanani tahadhari za mara kwa mara za Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki kwamba, nchi hiyo na waitifaki wake watafanya operesheni ya kijeshi dhidi ya makundi ya waasi wa Kikurdi kutoka Uturuki huko mashariki mwa Furati nchini Syria, Trump amefikia uamuzi kwamba, hapana budi kuliondoa jeshi la Marekani huko Syria ili kuepusha uwezekano wa kupigana majeshi ya nchi hiyo na yale ya Uturuki na kuzuia mivutano zaidi katika uhusiano wa Washington na Ankara.

Tukiachilia mbali sababu halisi ya uamuzi wa ghafla wa Rais Donald Trump wa Marekani wa kuliondoa jeshi la nchi hiyo huko Syria, serikali ya Damascus imekuwa ikisisitiza mara kwa mara kwamba, kuwepo kwa jeshi hilo katika ardhi ya Syria ni kinyume cha sharia na uvamizi unaopaswa kukomeshwa.