Tishio kali la Trump dhidi ya Uturuki
Baada ya Rais Donald Trump wa Marekani kutangaza hapo tarehe 19 mwezi Disemba mwaka jana uamuzi wa kuondoa askari vamizi wa nchi hiyo huko Syria, baadhi ya wachambuzi wa mambo waliuchukulia uamuzi huo kuwa sehemu ya juhudi zake za kutaka kuiridhisha Uturuki.
Kabla ya hapo Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki alikuwa ametangaza kwamba muda si mrefu angetuma askari wa nchi hiyo katika maeneo yanayodhibitiwa na Wakurdi wa Syria, hatua ambayo bila shaka ingehatarisha maisha ya askari wa Marekani walioko mashariki mwa Mto Furati. Mbali na hayo Marekani ilikuwa inafanya juhudi za kuishawishi Uturuki isinunue mfumo wa makombora ya S400 kutoka Russia na ndio maana mara tu baada ya kutangazwa uamuzi huo wa Trump, Washington ikatoa pendekezo la kuiuzia Uturuki mfumo wa makombora ya Patriot kwa thamani ya dola bilioni 3.5.
Ni wazi kuwa kutangazwa kuondoka askari wa Marekani nchini Syria lilikuwa pigo kubwa kwa washirika wa Kikurdi wa Washington, hivyo wakawa hawana budi ila kuomba msaada wa jeshi la Syria kwa ajili ya kukabiliana na shambulio lolote la Uturuki katika maeneo ya mashariki mwa Mto Furati. Katika toleo lake la tarehe 19 Disemba mwaka uliopita, gazeti la New York Times liliadika kuwa askari wa Kikurdi ndio wangekuwa washindwa wakubwa zaidi wa kuondolewa askari wa Marekani katika ardhi ya Syria.
Kwa kutilia maanani taathira mbaya za uamuzi wa Trump, baadhi ya washirika wa Ulaya wa Washington ikiwemo Ufaransa wametaka Marekani iendelee kuwaunga mkono Wakurdi. Inaonekana kuwa baada ya Trump kuchukua uamuzi wa ghafla wa kuondoa askari wa nchi yake huko Syria na bila kuzingatia hatima ya washirika wa Washington kaskazini mwa nchi hiyo, yaani Wakurdi na Wafuasi wa Demokrasia nchini Syria katika kukabiliana na hujuma tarajiwa ya Uturuki katika maeneo ya mashariki mwa Mto Furati, rais huyo amechuku auamuzi mgumu katika uwanja huo baada ya kushinikizwa na maafisa wakuu wa timu yake ya masuala ya usalama. Katika ujumbe ulioutuma katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter leo alfajiri, Trump ameashiria tishio la Uturuki kuwashambulia Wakurdi kaskazini mwa Syria na kusema kuwa nchi hiyo haipasi kutekeleza shambulio hilo. Ametishia kuwa iwapo Uturuki itatekeleza shambulio hilo, Washington itautokomeza uchumi wa nchi hiyo. Wakati huohuo, amewataka Wakurdi kutoichokoza Uturuki na kusisitiza kuwa serikali ya Washington itabuni eneo lisilo la kijeshi lenye ukubwa wa maili 20 (kilomita 30) katika eneo hilo.
Tishio hilo lisilo na mfano wake la Trump limeipelekea Uturuki kutoa onyo kali dhidi ya serikali ya Washington. Akizungumzia tishio hilo hivi karibuni, İbrahim Kalın, msemaji wa Rais Tayyib Erdogan amesema kuwa kuchukuliwa Wakurdi wote wa Syria kuwa sawa na wanamgambo wa Kikurdi, 'litakuwa ni kosa la kuangamiza.' Ameendelea kusema kuwa Uturuki inataraji kuwa Marekani itaheshimu uhusiano wake wa kistratejia na nchi hiyo. Amemuhutubu Trump kwa kusema: 'Magaidi hawapasi kuwa waitifaki na washirika wako.'
Inaonekana kuwa tishio hilo kali la Trump dhidi ya serikali ya Ankara limetolewa baada ya kufeli mazungumzo ya wiki iliyopita kati ya John Bolton, mshauri wa usalama wa taifa wa Marekani na maafisa wakuu wa Uturuki kuhusiana na uamuzi wa nchi hiyo wa kutaka kuwashambulia waamgambo wa Kikurdi wanaojulikana kama Vikosi vya Kuwalinda Wananchi, YPG. Uturuki imekuwa ikisisitiza mara kwa mara kwamba wanamgambo wa Kikurdi wa Syria wana uhusiano wa moja kwa moja na Chama cha Wafayakazi wa Kurdestan PKK ambapo wanawapa wafuasi wa chama hicho silaha ambazo wamepewa na Marekani kwa ajili ya kupambana na magaidi wa Daesh, na hivyo kuhatarisha usalama wa taifa ka Uturuki. Kwa mujibu wa kauli ya İbrahim Kalın, hakuna tofauti yoyote iliyopo kati ya chama cha PKK na Daesh.
Akizungumza na afisa mwenzake wa Uturuki hapo siku ya Jumanne, John Bolton alisema waziwazi kwamba Marekani inapinga moja kwa moja muamala wowote mbaya wa jeshi la Uturuki na washirika wa Kikurdi wa Washington nchini Syria, jambo ambalo limewakasirisha mno viongozi wa ngazi za juu wa Uturuki. Huku akiashiria matamshi yaliyotolewa na Bolton kuhusiana na kuondoka askari wa Marekani huko Syria, na hasa kuhusu onyo la kutoshambuliwa wanamgambo wa Kikurdi na askari wa Ankara, Rais Erdogan wa Uturuki imepinga vikali suala hilo na kusema kuwa Bolton alifanya 'kosa kubwa' kuhusiana na jambo hilo. Kwa kutilia maanani tishio lisilo na mfano wake la Trump dhidi ya Ankara, inaonekana kuwa uhusiano wa Uturuki na Marekani utaingia katika hatua mpya ya mgogoro.