Uturuki yasema haibabaishwi na vitisho vya Trump
Waziri wa Mambo ya Nje ya Uturuki Mevlüt Çavuşoğlu amesema nchi hiyo haibabaishwi wala kutiwa kiwewe na kauli ya vitisho ya Rais Donald Trump kwamba Marekani itausabababishia matatizo uchumi wa Ankara.
Çavuşoğlu amesema hayo leo Jumatatu na kuongeza kuwa, "Tumesema mara zote kuwa hatuogopi wala hatubabaishwi na vitisho vya aina yoyote."
Amebainisha kuwa, vitisho vya kuhujumu uchumi wa Uturuki havitafika popote.
Matamshi ya Waziri wa Mambo ya Nje ya Uturuki yametolewa siku moja baada ya Donald Trump kutishia kuwa, Marekani itavuruga uchumi wa Ankara iwapo itawashambulia magaidi wa Kikurdi wanaoungwa mkono na Washington, baada ya Marekani kudai kuwa imeanza kuondoa askari wake nchini Syria.
Msemaji wa Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki, Ibrahim Kalin hata hivyo amesisitiza kuwa Ankara itaendelea kupambana na makundi ya PKK na YPG inayoyatambua kuwa ni magenge ya kigaidi yasiyo na tofauti na Daesh (ISIS).
Tarehe 19 Disemba mwaka uliomalizika wa 2018, Trump alisema kuwa ataondoa wanajeshi wa Marekani nchini Syria katika kipindi cha siku 30, lakini baada ya matamshi yake kukumbwa na upinzani mkali alibadilisha msimamo na kusema atawaondoa polepole wanajeshi hao katika kipindi cha siku 120.