Kutimuliwa NATO, tishio lisilo na kifani la Marekani dhidi ya Uturuki
Uhusiano wa Marekani na Uturuki umekuwa mbaya katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita hasa baada ya jaribio la kuipindua serikali ya Rais Recep Tayyip Erdogan manamo Junia 15 mwaka 2016.
Baada ya kuingia madarakani Donald Trump kama rais wa Marekani mnamo Januari 20 2017, maafisa wa ngazi za juu wa Uturuki walikuwa na matumaini kuwa uhusiano nchi mbili utaboreka lakini kinyume na matarajio hayo, uhusiano umezidi kuvurugika.
Moja ya nukta muhimu ya hitilafu baina ya Marekani na Uturuki ni sisitizo la Uturuki la kununua mfumo wa S-400 wa makombora ya kujihami angani kutoka Russia.
Uturuki ni mwanachama wa muungano wa kijeshi wa Magharibi unaoongozwa na Marekani ujulakano kama Shirika la Mkataba wa Atlantiki ya Kaskazini (NATO). Kwa msingi huo Marekani inadai kuwa kuingia mfumo wa S-400 katika mfumo wa kujihami angani wa NATO ni jambo ambalo litaweka wazi udhaifu wa ndege za kivita za wanachama wa NATO hasa ndege aina ya F-35 ya Marekani.
Aidha serikali ya Trump ina wasiwasi kuwa, kununua silaha za Russia kutaifanya Uturuki iwe tegemezi kwa nchi hiyo inayotazamwa kuwa hasimu mkuu wa NATO. Kwa msingi huo wakuu wa Marekani wana wasiwasi kuwa jambo hilo litaifanya Uturuki iikaribie zaidi Russia na kutoa pigo kwa NATO.
Mbali na hayo, kuna baadhi ya weledi wa mambo wanaoamini kuwa Marekani ina wasiwasi mkubwa kutokana na kuwa mfumo wake wa makombora ya kujihami wa Patriot ni dhaifu mno mbele ya mfumo wa S-400 wa Russia.
Hatua ya Uturuki kununua S-400 si tu kuwa inapingwa vikali na Bunge la Marekani, Kongresi, na pia Wizara ya Ulinzi ya nchi hiyo, Pentagon, bali sasa pia serikali ya Marekani imechukua hatua za kivitendo kuizuia Uturuki kununua silaha hiyo ya kisasa kutoka Russia.
Siku ya Jumanne, Marekani ilichukua hatua ya kwanza ya kuizuia Uturuki kununua ndege za kivita aina ya F-35. Aidha Marekani imesema haitaiuzuia Uturuki vipuri vya ndege zake za kivita.
Halikadhalika Marekani imetoa tishio jingine lisilo na kifani dhidi ya Uturuki na kuhusiana na hilo Makamu wa Rais wa Marekani Mike Pence, siku ya Jumatano usiku aliashiria hatua ya Uturuki ya kuendelea kusisitiza kununua mfumo wa S-400 kutoka Russia na kutahadharisha kuwa: "Uturuki inapaswa kuchagua baina ya kusalia NATO au kununua S-400."
Akizungumza katika sherehe ya mwaka wa 70 wa kuanzishwa NATO, Pence alisema: "Uturuki inapaswa kuamua iwapo inataka kubakia kuwa mshirika muhimu katika NATO au inataka kuangamiza shirika hili kwa maamuzi yake yasiyo ya uwajibikaji."
Makamu wa Rais wa Marekani amesisitiza kuwa, nchiwanachama wa NATO hazipaswi kununua silaha za madola adui.
Kwa msingi huo makabliano ya Marekani na Uturuki kuhusu kadhia ya kununua mfumo wa makombora ya kujihami ya S-400 yameingia awamu mpya ambapo Washington inatoa vitisho vya kutimuliwa Uturuki kutoka NATO. Tishio hilo limeiweka Uturuki katika hali ngumu sana.
Pence ametoa matamshi hayo katika hali ambayo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglu akiwa safarini mjini Washington amesema kwa yakini nchi yake itanunua mfumo wa S-400 kutoka Russia.
Katika miezi ya hivi karibuni Marekani imeitahadharisha Uturuki kuhusu kununua mfumo huo wa makombora kutoka Russia.
Charles Summers, Msemaji wa WIzara ya UIinzi ya Marekani, Pentagon, hivi karibuni alitangaza kuwa: "Matokeo ya Uturuki kununua S-400 yatakuwa ni hatari sana. Kwa kununua mfumo wa makombora ya kijihami wa S-400 kutoka Russia, Uturuki ifahamu kuwa haitaweza kupata ndege za kivita za F-35 na mfumo wa makombora ya Patriot.
Kwa mtazamo wa viongozi wa Uturuki, akiwemo Rais Erdogan, Marekani ina mtazamo wa undumakuwili kuhusu kadhia hii.
Anasema katika hali ambayo nchi zingine za NATO kama vile Bulgaria, Ugiriki na Slovenia zinatumia mfumo wa makombora ya kujihami wa S-300 kutoka Russia, lakini Marekani haizishinikizi huku ikiendelea kuishinikiza Uturuki isinunue S-400.
Pamoja na hayo, si tu kuwa Uturuki inasisitiza kuhusu kununua mfumo huo wa S-400 bali pia imesema iko tayari kununua mfumo wa kisasa na bora zaidi wa S-500 kutoka Russia.